1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wasema saa ya Mubarak "kukata roho" imefika

Abdu Said Mtullya3 Februari 2011

Wahariri wazungumzia juu ya mapambana ya jana mjini Cairo.

https://p.dw.com/p/109o7
Waandamanaji wakisema "Mubarak nenda zako!"Picha: AP

Matukio ya nchini Misri bado yanaendelea kugonga vichwa vya habari duniani. Na nchini Ujerummani wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya matukio hayo.

Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung anaesema kuwa waandamanaji wanaotetea demokrasia wameonyesha wazi kwamba hawakubali kubabaishwa na ahadi iliyotolewa na rais Mubarak kwamba hatagombea tena urais mnamo mwezi wa septemba. Gazeti hilo linasema waandamanaji wanaotetetea demokrasia wanamtaka Mubarak aondoke mara moja. Lakini badala yake utawala wake jana ulianza kuwashambulia watetezi wa demokrasia kwa kuwatumia mawakala wanaonufaika na utawala huo.

Mhariri wa gazeti la Hessische/Niedersächsiche Allgemeine pia anazungumzia juu ya mashambulio yaliyofanywa jana na mawakala wa utawala wa rais Mubarak.

Mhariri huyo anasema kuwa Mubarak sasa anatumia kila mbinu ili kuwakabili wapinzani wake.Mhariri huyo anaeleza kwamba Rais Mubarak anataka dunia ione kwamba sasa pana makundi mawili ya umma wa Misri yanayopingana. Lakini licha ya utepetevu wa wanajeshi, mhariri anasema jambo moja ni wazi, nalo ni kwamba saa haiwezi kurudi nyuma tena nchini Misri. Hata hivyo, wanajeshi wanaweza kusaidia katika kuepusha umwagikaji wa damu.

Gazeti la Braunschweiger linawazungumzia wale wanaomuunga mkono Rais Mubarak waliojitokeza jana na kupambana na wapinzani wa serikali. Gazeti hilo linaeleza kuwa wanaomuunga mkono Mubarak ni wale wanaonufaika na utawala wake, lakini watu hao siyo wawakilishi wa umma. Gazeti hilo linasema kuwa maamlaka ya Mubarak yamo hatarini kuondoka. Na wapo wengi ambao kwa muda wa miaka mingi wamekuwa wananufaika na utawala wa Mubarak-wale ambao wamekuwa wanajitajirisha .Lakini hao siyo wanaowakilisha matumaini. Ni wapinzani wa Mubarak wanaowakilisha mustakabali wa matumaini.

Mashabiki wa Mubarak hawatimii hata milioni moja na wala hawauwakilishi umma wa Misri.

Mhariri wa gazeti la Badische Neueste Nachrichten anasisitiza kuwa safari ya Mubarak ya kupotelea mbali,ilianza siku nyingi, kiasi kwamba gurudumu la historia haliwezi kurudi nyuma tena! Mhariri huyo anaeleza kwamba Misri imesimama ana kwa ana na mustakabali. Pana fursa mpya. Lakini pia bado pana hali ya wasiwasi. Siku zinazokuja zitaonyesha wazi wapi Misri inaelekea.


Katika maoni yake gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya msimamo wa Marekani, kwa kusema kwamba utawala wa Obama umegawika katika sehemu mbili juu ya matukio ya nchini Misri. Mhariri huyo anafafanua kwa kusema"Utawala wa Obama haujatamka kadamnasi kumtaka rais Mubarak andoke madarakani, badala yake rais Obama aliyasema hayo kwa njia ya simu." Gazeti hilo linaeleza kuwa hayo yanaonyesha mgawanyiko wa haiba ya Marekani juu ya mgogoro wa Misri. Lakini gazeti linakumbusha kuwa yaliyotokea Iran miaka zaidi ya 30 iliyopita yanapasa kuwa onyo na funzo kwa Marekani. Marekani inapaswa kusimama wazi katika upande sahihi wa historia.

Mwandishi/Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman