1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wasifu ziara ya Merkel Afghanistan

Abdu Said Mtullya13 Machi 2012

Wahariri karibu wote wanazungumzia juu ya Afghanistan baada ya mkasa wa kuuliwa raia 16 na askari wa Marekani.Wahariri hao wanatilia maanani kuwa Merkel alienda Afghanistan licha ya mkasa huo kutokea.

https://p.dw.com/p/14K2G
Kansela Merkel nchini Afghanistan
Kansela Merkel nchini AfghanistanPicha: dapd

Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" anatilia maanani kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewatembelea askari wa Ujerumani nchini Afghanistan licha ya mkasa huo. Mhariri huyo anaeleza kuwa ni hatari wakati wote kufanya ziara nchini Afghanistan. Lakini anasema ni muhimu kwamba Kansela Merkel ameifanya ziara hiyo, kwani vinginevyo dunia ingelipokea ishara kwamba hali ya Afghanistan haijadhibitika. Hata hivyo gazeti la"Mitteldeutsche Zeitung" linatilia maanani kuwa Kansela Merkel amekiri kwamba hali ya Afghanistan ni ngumu

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine  " linazitaka nchi za magharibi zijiulize  kwa makini;  nini kinaweza kutimizwa  kwa uhakika, nchini Afghanistan hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2014 ?Mhariri wa gazeti hilo anasema baada ya kulipata jawabu linaloonyesha  kwamba mambo hayaendi vizuri ,itakuwa sahihi kuanza kufanya mipango ya kuondoka. Watu wa Afghanistan ,anasema hawatapaswa kulalamika juu ya mipango hiyo. Sababu ni kwamba Waafghani wenyewe wanatoa mchango mdogo katika kuujenga mustakabal wa nchi yao.. Mhariri huyo amezitaka nchi za magharibi ziumalize mchezo wa  patapotea zinaoucheza nchini Afghanistan .

Lakini mhariri wa "Westdeutsche  Zeitung" anasema baada ya askari wa Marekani kuwaua raia 16,ni jambo la uhakika kwamba moto utawaka nchini  Afghanistan. Kansela Merkel anayatambua hayo na ndiyo sababu hajatoa kauli ya uwazi juu ya terehe ya kuondolewa majeshi ya Ujerumani kutoka Afghanistan. Mhariri wa "Westdeutsche Zeitung" anaeleza kuwa Kansela Merkel hajaitamka wazi tarehe ya kuyaondoa majeshi ya Ujerumani kutoka Afghanistan.

Pia alirejea haraka kutoka Afghanistan baada ya kuyatembelea majeshi ya Ujerumani. Pana sababu mbili. Kwanza anatambua kwamba vita vya Afghanistan haviungwi mkono sana na Wajerumani. Jambo la pili ni kwamba Ujerumani siyo nchi yenye usemi mkubwa kwenye mfungamano wa nchi zilizochangia majeshi nchini Afghanistan. Wenye usemi mkubwa ni Wamarekani ambao hawafikirii kuurefusha muda wa uwepo wa majeshi yao katika vita ambavyo hawawezi kushinda.

Mhariri wa gazeti la "Donaukurier" anatoa maoni juu ya mgogoro wa nchini Syria. Anasema wakati wa kuleta mwafaka umeshapita nchini humo.Mhariri huyo anahoji kwamba ama Rais Assad aendelee kufanya ukatilii mpaka ashinde au atimuliwe. Hakuna njia nyingineLakini utawala wake unayumba. Kwa hivyo anasema mhariri wa Donaukurier " ikiwa jumuiya ya kimataifa itazungumza kwa kauli moja, njia ya Rais Assad itafikia mwisho haraka.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef