1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WAHARIRI WATOA MAONI JUU YA MKUTANO WA MERKEL NA SARKOZY

Abdu Said Mtullya17 Agosti 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wauzungumzia mkutano wa jana baina ya Kansela Merkel na Rais Sarkozy.

https://p.dw.com/p/12IDh
Kansela Merkel na Rais Sarkozy mjini ParisPicha: dapd

Magazeti ya hapa nchini leo yanatoa maoni juu ya mkutano wa kilele baina ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.

Magazeti hayo pia yanazungumzia juu ya matukio ya nchini Misri, Syria na Tunisia.

Juu ya mkutano wa jana mjini Paris baina ya Kansela Merkel na Rais Sarkozy gazeti la Braunschweiger linalitilia maanani pendekezo la viongozi hao juu ya kuanzisha kinachoitwa serikali ya kiuchumi. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema pendekezo hilo bado lipo mbali sana na hali halisi. Kwa sasa halina uhalali wa kidemokrasia.

Mhariri wa Badische Zeitung anasema pendekezo juu ya kuanzisha kinachoitwa serikali ya kiuchumi bado ni wazo tu linaloiishia katika mikutano ya viongozi wa Ulaya.Lakini ili lifanikiwe pendekezo hilo linahitaji mambo mawili. Kwanza lazima iwezekane kwa nchi za Ulaya kuliweka katika katiba, suala la kuziwekea serikali kikomo cha kukopa. Na jambo la pili ni kwamba nchi zote za Ulaya lazima ziutambue umuhimu wa kuanzisha kodi ya mabenki

Gazeti la Hessische/Niedersächische Allgemeine linaitilia maanani kauli ya Kansela wa Ujerumani kutoka kwenye mkutano wa jana kwamba mgogoro wa madeni barani Ulaya hauwezi kutatuliwa kwa mpigo! Mhariri wa gazeti hilo anasema baadhi ya kauli zilizotolewa na Kansela Merkel na Rais Sarkozy kwenye mkutano wao wa jana zilikuwa zimefunikwa na mawingu. Lakini Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema jambo sahihi kabisa, kuwa haiwezekani kuutatua mgogoro wa madeni barani Ulaya kwa pigo moja.Mhariri huyo pia anatilia maanani kwamba yaliyotamkwa na viongozi hao wawili, yamejenga imani kubwa katika jumuiya ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Sasa ni juu ya Ulaya kuonyesha nini inaweza kufanya.

Gazeti la General Anzeiger linasema Dhamana za pamoja zitakuja barani Ulaya licha ya msimamo wa Kansela Merkel wa kuzipinga hati hizo.! Mhariri wa gazeti hilo anasema ukweli huo haukwepeki.Anasema mchakato wa kuhawilisha fedha katika Umoja wa sarafu ya Euro tayari upo siku nyingi. Hayo yanapaswa kuonekana wazi kwa Kansela Merkel kama mwangaza wa jua Mhariri huyo anaeleza kuwa kwa sasa Kansela Merkel anasita kuliwasilisha wazo hilo kwa wajerumani kwa sababu anahofia kukipoteza kiti chake cha ukansela.

Gazeti la Honneversche Allgemeine linatoa maoni juu ya matukio ya Libya, Syria na Misri. Mhariri wa gazeti hilo anasema ni watu wa nchi hizo tu, wenye haki ya kuamua juu ya kuleta uhuru wao. Kwa hiyo nchi za magharibi na nchi za Nato zinatafuta nini katika mapinduzi ya nchi za kiarabu.?

Mwandishi/Mtullya Abdu/ Deutsche Zeitungen/

Mhariri/- Josephat Charo /