1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri watoa maoni juu ya ripoti ya Umoja wa Mataifa

Abdu Said Mtullya7 Julai 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wakasirishwa na ripoti ya Umoja wa Mataifa!

https://p.dw.com/p/11quJ
Wasiokuwa na makaazi katika jiji la FrankfurtPicha: picture alliance/ dpa


Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanaizungumzia ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya kijamii nchini Ujerumani.

Katika ripoti hiyo Umoja wa Mataifa umeilaumu vikali Ujerumani kuhusu sera zake za ajira, huduma za afya na usalama wa kijamii kwa wahamiaji. Ripoti hiyo pia inasema pana umasikini nchini Ujerumani licha ya utajiri mkubwa uliopo.

Mhariri wa gazeti la Dresdner Neueste Nachrichten anasema Umoja wa Mataifa umezidisha chumvi katika ripoti hiyo kwani inatoa picha ya kuonyesha kana kwamba nchini Ujerumani pana umasikini, kama katika Burkina Faso, Sudan au Guatemala.

Juu ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa mhariri wa gazeti la Allgemeine Zeitung anakumbusha enzi za Ujerumani Mashariki ya zamani, ambapo televisheni ya nchi hiyo ilionyesha picha za mabaya tu juu ya Ujerumani magharibi. Mhariri huyo anaeleza kwamba lengo la televisheni ya Ujerumani Mashariki wakati huo lilikuwa linaeleweka-kuonyesha mabaya tu juu ya mfumo wa kibepari. Lakini kwa taasisi inayoheshimika kama Umoja wa Mataifa, kutoa ripoti kama hiyo juu ya Ujerumani ni utobwe wa hali ya juu!

Gazeti la Märkische Oderzeitung linasema siyo jambo la kushangaza, kwa kamati ya masuala ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni ya Umoja wa Mataifa kutoa ripoti kama hiyo juu ya Ujerumani, kwa sababu katika kamati hiyo wapo wajumbe wanaotoka India, China na Urusi. Wananchi wa nchi hizo wangelifurahi, laiti wangelikuwa na matatizo kama yale yanayowakabili watu nchini Ujerumani. Kwani wananchi wa Ujerumani wanayo haki ya kupeleka mashtaka hata mbele ya Mahakama Kuu ili kudai haki zao. Ripoti iliyotolewa na kamati husika inaonyesha yapo mambo fulani yaliyofichamafichama katika mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Mhariri wa Stuttgarter Nachrichten anasema ripoti ya Umoja wa Mataifa inafanana na orodha ya vitu ambavyo mtoto mdogo anaviomba kutoka kwa wazazi wake lakini bila ya kujua fedha zitatoka wapi ! Mhariri huyo anafafanua kwamba Ujerumani ni nchi tajiri sana duniani. Bajeti yake ya kijamii ni kubwa mno, inayomeza nusu ya bajeti yote ya nchi. Lakini wakati huo huo deni la serikali linazidi kuongezeka. Kutokana na hoja hizo inahalisi, kusema kuwa ripoti ya Umoja wa Mataifa ni sawa na matamanio ya mtoto mdogo.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/ - Yusuf Saumu