1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WAHARIRI WATOA MAONI JUU YA WAKWEPA KODI

Abdu Said Mtullya11 Agosti 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wasema wakwepa kodi lazima wachague kati ya uadilifu na uhalifu!

https://p.dw.com/p/12F0O
Waziri wa fedha waUjerumani Wolfgang Schäuble.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya Ujerumani na Uswisi juu ya kuwakabili wakwepa kodi. Na pia wanazungumzuia juu ya ghasia za nchini Uingereza.

Baada ya muda mrefu ,Ujerumani na Uswisi hatimaye zimefikia makubaliano. Kulingana na makubaliano hayo wajerumani walioukuwa wanaficha fedha zao kwenye mabenki ya Uswisi watapewa fursa ya kulipa kwa siri malimbikizo ya kodi ya muda mrefu.

Juu ya mapatano hayo mhariri wa Die Badische Zeitung anatoa maoni yake, kwanza kwa kusema kuwa Wajerumani wangelipendelea kujua ni kiasi gani cha fedha ambacho wakwepa kodi wa Ujerumani wamekificha katika mabenki ya Uswisi. Kwa nini serikali ya Ujerumani haikusisitiza jambo hilo. Ni kweli kwamba baada ya muda mrefu makubaliano yamefikiwa, lakini watu wanataka kujua ,ni kiasi gani cha fedha kinachozungumziwa.

Naye mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anasema sasa ni juu ya wahalifu waliokuwa wanakwepa kulipa kodi kuitumia fursa waliyopewa ili kujiepusha na adhabu. Mhariri huyo anaeleza kuwa wakwepa kodi wa Ujerumani sasa wanapaswa kuchagua, kurejea katika uadilifu ama kuendelea kuzama katika uhalifu . Makubaliano yaliyofikiwa baina ya serikali za Ujerumani na Uswisi yanatoa fursa kwa watu hao ya kusema ukweli. Hata hivyo mhariri wa gazeti la Rhein Neckar anatilia maanani kwamba, kufikiwa makubaliano hayo hakuna maana kuwa wakimbizi wa kodi watatoweka kwenye mabenki ya Uswisi. Mhariri huyo anasema wakimbizi hao hawatatoweka . Anaeleza kuwa kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa utaratibu wa kuficha siri za wateja utaendelea kwenye mabenki ya Uswisi, lakini kuanzia sasa wakweka kodi hao hawatakuwa na utulivu.

Gazeti la Handelsblatt linatoa maoni juu ya ghasia zinazoendelea nchini Uingereza. Gazeti hilo linasema kwamba vurumai zinazofanywa na vijana zinaonyesha kuwa vijana hao wanapigania hadhi-wanataka kutambuliwa kuwa muhimu katika jamii. Mhariri wa gazeti hilo anaendelea kueleza kuwa heshima ndiyo wanayoitaka vijana hao wa Uingereza. Yeyote anaehisi kuwa hathaminiwi na jamii yake, basi yeye pia hatathamini hata mali za wanajamii wengine, na wala hatawathamini watu wengine.

Naye mhariri wa Dithmarscher Landeszeitung,anatilia maanani kauli zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani juu ya machafuko ya nchini Uingereza. Wanasiasa hao wa vyama vya CSU na SPD wamesema haraka sana, kwamba yanayotokea sasa nchini Uingereza hayawezi kutokea nchini Ujerumani. Lakini mhariri huyo amewakariri wanasiasa wa chama cha mrengo wa shoto waliotoa kauli ya nadhari,kwa kueleza kuwa vijana wanaofanya ghasia nchini Uingereza hawana hatia. Wenye hatia ni wale waliowasukumia vijana hao pembezoni mwa jamii.

Mwandishi/Mtullya/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman.