1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza wakimbilia vyakula vinavyokuzwa nchini mwao

Josephat Charo7 Februari 2007

Maduka makubwa ya bidhaa nchini Uingereza yanang´ang´ania kuvutia mamilioni ya fedha kutoka kwa wateja waliohamasishwa kuhusu mazingira. Maduka ya wakulima nchini Uingereza yanavamiwa na wateja wanaozingatia ununuzi wa vyakula vinavyokuzwa kwenye mashamba nchini humo na kupelekwa sokoni moja kwa moja baada ya kuvunwa. Mwenendo huu huenda ukaathiri ununuzi wa vyakula kutoka mataifa ya kigeni nchini humo.

https://p.dw.com/p/CHKa
Matunda na mboga katika masoko ya Uingereza
Matunda na mboga katika masoko ya UingerezaPicha: NürnbergMesse

Huku tatizo la ongezeko la joto duniani likiendelea kugonga vichwa vya habari, Waingereza wameamua kununua vyakula ambavyo havijakaa kwa muda mrefu wanapokwenda madukani. Mawazo yao yamekita katika mwendo vyakula vinaolazimika kusafiri kabla kufika kwenye masoko ya Uingereza.

Bill Vorley, kiongozi wa kitengo kinachohusika na masoko endelevu katika taasisi ya kimataifa ya mazingira na maendeleo nchini Uingereza, IIED, amesema Waingereza wengi wanazingatia sana vyakula vinakotokea kabla kuvinunua. Wateja wanapendelea kununua vyakula ambavyo vimesafiri mwendo mfupi kutoka shambani hadi kufikia mezani tayari kwa kula. Hata hivyo huku wateja wakitaka kupunguza mwendo mrefu wa vyakula, baadhi ya wataalamu wameonya kwamba wazo hilo huenda lisababishe athari nyingi mno badala ya kuleta faida.

Wataalamu hao wamewaomba wabunge kutoanzisha kampeni kuwataka watu wanunue vyakula vinavyokuzwa ndani ya Uingereza, hatua ambayo huenda ikawa pigo kubwa kwa wakulima masikini barani Afrika. Bill Vorley anasema yeye anaunga mkono ununuzi wa vyakula vinavyokuzwa nchini Uingereza lakini ameonya dhidi ya kutumia mazingira kuukwamisha uchumi, hususan ikizingatiwa kwamba uamuzi ya wateja na viongozi wanaohusika katika kuunda sera hautasaidia kupunguza kiwango cha gesi ya carbon dioxide katika anga ya Uingereza.

Kwa mujibu wa baraza la kitaifa la wateja la Uingereza, NCC, takriban asilimia 10 ya gesi ya carbon dioxide inayotokana na usafirishaji wa vyakula hutoka kwenye bidhaa zinazohifadhiwa kutumia gesi. Katika ripoti yake ya hivi karibuni baraza hilo lilisema gesi ya carbon dioxide inayoingia katika anga ya Uingereza kutoka kwa mkebe mmoja wa matunda uliosafirishwa kutoka New Zealand hadi Uingereza ni sawa na gesi inayotolewa katika safari kumi za wazazi wanaowapeleka watoto wao kutumia motokaa zao.

Wataalamu wanasema tatizo lililopo ni kwamba wateja wanataka kuonyesha wanayajali mazingira kwa kununua vyakula bila kufahamu mjadala huu. Wanatumia tu wazo kuwa vyakula vya Uingereza ni bora zaidi kuliko bidhaa kutoka nchi nyingine. Ni Waingereza wachache walio tayari kununua vyakula vilivyo na alama kuonyesha vinatoka New Zealand au Kenya.

Wateja wanatakiwa wazingatie kwa makini kabla kuamua ni bidhaa gani wanazotaka kununua. Matunda na mboga kutoka Afrika, ambazo Waingereza hutumia zaidi ya paundi milioni moja kila siku, zinatakiwa kuzingatiwa kwa makini. Harriet Lam, mkurugenzi mtendaji wa wakfu wa Fairtrade, amesema bidhaa nyingi kutoka Afrika huwapa watu maskini kutoka mataifa maskini fursa ya kuishi maisha mazuri. Lamb na Vorley wamesema kupiga marufuku bidhaa kutoka Afrika kutapunguza kiwango cha gesi ya carbon dioxide duniani kwa asilimia 0.1.

Stephen Mbugua, naibu mwenyekiti wa shirika la kuuza bidhaa katika mataifa ya kigeni mjini Nairobi Kenya, amesema hali mpaka sasa si mbaya, lakini kama kampeni itafanywa, huenda kukawa na athari mbaya katika siku za usoni.

John Kanjangaile, meneja anayehusika na uuzaji wa bidhaa katika mataifa ya kigeni kwenye ushirika wa mjini Kagera, amenukuliwa akisema kwenye mkutano uliofanyika mjini London kwamba wakaazi wa mataifa ya magharibi wasiwasukumie wakulima maskini mzigo wa kulipa gharama kwa matatizo ya mazingira yanayosbabishwa na mataifa hayo.