1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waingereza wapiga kura

7 Mei 2015

Wananchi wa Uingereza wanapiga kura katika uchaguzi wenye ushindani mkali ambao huenda matokeo yake yakaunda serikali dhaifu na kuisukuma nchi hiyo kukaribia hatua ya kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1FM8e
Mjadala wa Televisheni wa viongozi wa vyama nchini Uingereza
Mjadala wa Televisheni wa viongozi wa vyama nchini UingerezaPicha: Ken McKay/ITV/Handout via Reuters

Uchunguzi wa mwisho wa maoni ya wananchi wa Uingereza umeonyesha kwamba chama cha waziri mkuu David Cameron cha kihafidhina na kile cha upinzani Labour kinachoongozwa na Ed Milliband vinakwenda sambamba katika kuungwa mkono na wananchi ishara ambayo ni dhahiri hakuna kitakachoweza kushinda moja kwa moja wingi wa viti vya bunge lenye viti 650.

Kiongozi wa chama cha Labour Ed Milliband
Kiongozi wa chama cha Labour Ed MillibandPicha: AFP/Getty Images/O. Scarff

Katika mkesha wa kuamkia uchaguzi wa leo Ed Milliband kiongozi wa chama cha Labour alisema mbele ya wafuasi wake huko Pendle kaskazini mwa nchi kwamba kinyang'anyiro kitakuwa kigumu mno kiasi ambacho haijawahi kuonekana,huku waziri mkuu Cameron nae akisema ni chama chake pekee kinachoweza kuleta serikali imara katika taifa hilo.

Cameron amesema vyama vingine vyote vinaweza kusababisha matatizo.Chama cha kihafidhina kinajinadi kama chama chenye uwezo wa kuunda nafasi za ajira pamoja na kuufufua uchumi kikiahidi kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwa watu milioni 30 huku kikiahidi pia kupunguza zaidi matumizi kwa lengo la kuondoa nakisi ya bajeti ambayo hadi sasa iko katika kiwango cha asilimia 5 ya pato jumla la ndani.

Chama cha Labour kwa upande wake kinasema kitapunguza nakisi ya bajeti ya nchi kila mwaka na kuongeza kodi ya mapato kwa moja asilimia kwa wenye mishahara mikubwa na kutetea maslahi ya familia za watu wanaofanya kazi lakini wanakabiliwa na hali ngumu ya kifedha katika kumudu bima ya afya ya taifa.

Endapo hakuna chama kitakachoshinda kwa wingi wa viti mazungumzo ya kuunda serikali yanatarajiwa kuanza ijumaa ambapo vyama vidogo vitaanza mchakato ya kufikia makubaliano.Mchakato huo huenda ukafikia hatua ya kuundwa serikali ya muungano kama ile ambayo waziri mkuu Cameron amekuwa akiiongoza miaka mitano iliyopita akiwa na Liberal Demokrats au huenda ikapatikana serikali dhaifu ya wachache.

Kiongozi wa Wahafidhina David Cameron
Kiongozi wa Wahafidhina David CameronPicha: C. Somodevilla/Getty Images

Wakati upigaji kura ukiendelea katika vituo mbali mbali nchini humo vyama vikuu viwili Wahafidhina na Labaour vinakaribiana kabisa kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa miezi kadhaa,ambapo wahafidhina wanaongoza kwa 1 asilimia ingawa uchunguzi mwingine wa maoni umeonyesha Labour wanaongoza kwa asilimia 2.

Ikiwa uchunguzi huo wa maoni ndio hali halisi ya mambo yatakavyokuwa basi hapana shaka vyama hivyo vitalazimika kuungwa mkono na alau vyama viwili vidogo kuunda serikali,lakini tayari chama kikuu cha Scotland SNP kinachotarajiwa kupata ushindi wa kishindo Scotland, kimeshaondoa uwezekano wa kufikia makubaliano aina yoyote na David Cameron.Ingawa pia Ed Milliband kiongozi wa chama cha Labour amefuta uwezekano wa kuungana na SNP ,Na ikiwa hatua ya kuunda serikali imara itashindikana Uingereza inaweza ikajikuta katika mvutano wa kisiasa na hata uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya uchaguzi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba