1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wairaq watathmini uvamizi

12 Machi 2008

Miaka mitano baada ya vikosi vya Marekani na Uingereza kuingia nchini Iraq na kumpinduwa Saddam Hussein wananchi wengi wa Iraq wanauliza iwapo umwagaji damu na machafuko yaliovuruga maisha yao yanastahiki uvamizi.

https://p.dw.com/p/DN0E
Nembo ya Iraq ya kesho

Kwa mujibu wa makadirio mbali mbali idadi ya raia waliopoteza maisha yao nchini humo ni kubwa mno kati ya watu 90,000 hadi milioni moja,takriban wanajeshi wa Marekani 4,000 wameuwawa wakati Wairaq milioni nne wamepoteza makaazi yao.

Mohamed Dahman anasimulia zaidi juu ya tathmini ya Wairaq miaka mitano baada ya uvamizi ulioongozwa na Marekani.

_______________________________________

Kwa upande unaonekana kuwa mzuri ni kwamba Wairaq wameondokana na mmojawapo wa madikteta wa kikatili kabisa wa karne ya 20. Wameweza kufanya uchaguzi huru na kuwa na katiba mpya.

Kwa wananchi wa Iraq kuamuwa iwapo uvamizi huo unastahiki kutolewa muhanga kwao kunategemea kwa kiasi fulani madhehebu na ukabilia pamoja na mahala wanakoishi.

Saddam muarabu wa madhehebu ya Sunni aliwakandamiza Washia walio wengi nchini humo na Wakurdi.Washia hivi sasa wanashikilia hatamu za madaraka wakati Wasunni waliokuwa wakitawala nchi hiyo sasa wametengwa.

Mjini Baghdad kitovu cha vita vya vya kikabila vya mwaka 2006 na 2007 ambavyo nusura viigawe nchi hiyo watu wanatamani kuwepo kwa mitaa yenye usalama iliokuwepo wakati wa enzi ya Saddam. Kwa upande wa kusini walioko Mashia hawahofii tena magenge ya Saddam lakini makundi hasimu ya Mashia yanawania udhibiti.

Kwa upande wa kaskazini uchumi wa jimbo linalojiendesha wenyewe kwa kiasi kikubwa la Kurdistan unanawiri katika eneo ambalo Wakurdi wanaita Iraq nyengine.

Waziri wa mambo ya nje Hoshiyar Zebari ambaye ni Mkurdi anasema Iraq inaelekea njia sahihi na kwamba wale wanaosema uvamizi huo ulikuwa ni kosa wanapaswa kukumbuka ukatili wa Saddam Hussein.

Um Khalid msusi mjini Baghdad mwenye umri wa miaka 40 anasema umwagaji damu umekuwa holela sana kiasi kwamba hakuna anayejuwa wakati gani anaweza kuwa muhanga na kwamba kilichotokea nchini humo hakistahiki na wale wanaosema mambo mazuri wanadanganya.

Uhuru mpya na matumaini kwamba Marekani itaigeuza Iraq kuwa nchi nyengine ya kitajiri ya Kiarabu huko Ghuba yalivunjika wakati Waarabu wa madehebu ya Sunni waliposimama kidete dhidi ya watawala wao wapya na mabomu yaliotegwa kwenye magari yakaugeza masoko na misikiti kuwa medani za mauaji.

Hapo mwezi wa Februari mwaka 2006 wanamgambo wanaotuhumiwa kuwa wa kundi la Al Qaeda waliuripua msikiti mtakatifu wa Washia katika mji wa Samarra na kuzusha wimbi la umwagai damu wa kikabila ambalo likamanisha kwamba kuwa Mshia au Msunni kwenye kitongoji usikostahiki kunaweza kuwa hukumu ya kifo kwako.

Abu Wassan mwenye umri wa miaka 55 brigedia generali wa zamani na mwanachama mwandamizi wa chama cha Baath cha Saddam kilichopigwa marufuku anakiri kwamba kabla ya mwaka 2003 walikuwa wakiishi chini ya utawala mkali lakini katu hawakuwahi kusikia juu ya maiti kutupwa kwenye taka kwa sababu tu ya watu kuwa na majina ya Kisuni au Kishia.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba Wairaq milioni nne wanahangaika kujitafutia riziki wakati asilimia 40 ya watu milioni 27 wa nchi hiyo hawana maji safi ya kunywa.

Baadhi ya Wairaq wana hofu kwamba uvamizi umechochea kujichomoza kwa vikundi vya kisiasa ambavyo vinaweza kusababisha kugawika kwa Iraq baina ya maeneo ya Washia,Wasunni na Wakurdi na hiyo uwezekano wa umwagaji damu usioweza kuepukwa ambao yumkini ukazingiza hata nchi jirani.