1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisraeli wapiga kura

17 Machi 2015

Maaafisa wa uchaguzi wanasema idadi ya wapiga kura waliojitokeza ni kubwa ikilinganishwa na chaguzi zilizopita,Netanyahu akiwataka wafuasi wake kumuunga mkono kuzuia anachokiita kitisho cha usalama wa taifa la kiyahudi.

https://p.dw.com/p/1EsEL
Waziri mkuu Benjamin Netanyahuakipiga kura yake
Waziri mkuu Benjamin Netanyahuakipiga kura yakePicha: picture-alliance/AP Photo/Sebastian Scheiner

Waisrael wanaendelea na zoezi la upigaji kura katika uchaguzi muhimu wa bunge utakaoamua hatma ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu madarakani. Kufikia saa nne asubuhi ya leo,(17.03.2015) asilimia 14 ya watu walikuwa wameshapiga kura. Mtandao wa kijamii wa Facebook ulitawaliwa na ujumbe uliosema nimepiga kura kwa lugha ya kihibrew ujumbe ambao umezoeleka katika chaguzi zinazofanyika kwenye nchi nyingine nyingi kama juhudi za kuwavutia wapiga kura kujitokeza kwa wingi.

Kimsingi katika siku hii ya uchaguzi ni siku ya mapumziko nchini Israel na watu wengi hawendi makazini, na badala yake fukwe za bahari na mikahawa hufurika watu huku pia maduka yakiuza bei nafuu kwa ajili ya siku hii.

Waziri mkuu anaemaliza muhula wake nchini Israel, Benjamin Netanyahu, amewatolea wito wafuasi wa siasa kali nchini humo wateremke kwa wingi vituoni, akisema kuwa kuteremka kwa wingi kwa Waisrael wenye asili ya Kiarabu vituoni kunahatarisha ushindi wa mrengo wa kulia.

Tzipi Livni akipiga kura na wenzake wa muungano wa kizayuni
Tzipi Livni akipiga kura na wenzake wa muungano wa kizayuniPicha: Getty Images/GALI TIBBON

Uchunguzi wa maoni ya umma unaashiria matokeo yaliyokaribiana sana kati ya chama chake cha kihafidhina cha Likud na kile cha mrengo wa kati kushoto - Umoja wa Uzayuni - huku chama hiki kinachoongozwa na Isaac Herzog kikiongoza.

Wapigakura wanachaguwa wawakilishi wa bunge 120 katika orodha ya vyama mbali mbali vya kisiasa na sio mtu binafsi. Hakuna chama ambacho kimewahi katika historia ya nchi hiyo kushinda moja kwa moja kwa wingi mkubwa wa viti bungeni na na kwahivyo baada ya uchaguzi huu inaweza kuchukua wiki kadhaa ya kufanyika mashauriano ya kuunda serikali ya mseto ya vyama kadhaa.

Vyama vingi vidogo vidogo vinavyoegemea upande wa kati na vile vya kidini ambavyo vimeshaahidi kumuunga mkono ama Netanyahu au Herzog huenda vikaanza kuashiria wizani unaegemea wapi kuamua nani atakuwa waziri mkuu ajae.

Ikumbukwe kwamba katika hatua ya kushangaza ya dakika za mwisho mwisho ya kujaribu kuwavutia wapiga kura kuelekea kambi yake ya mrengo wa kulia Netanyahu jana usiku aliahidi kuzuia uundwaji wa dola la Wapalestina na kuwashutumu wapinzani wake kwa kuhatarisha usalama wa nchi hiyo kwa kutafuta amani na majirani zao Waarabu. Lakini mpinzani wake Herzog amejibu shutuma hizo akiwambia Waisraeli kwamba anayetaka mabadiliko, matumaini na hatma njema kwa Waisraeli atachagua muungano wa Kizayuni anaouongoza.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef