1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajamaica watamba katika riadha

Mohmed Dahman22 Agosti 2008

Jamaica hapo jana imejizolea vizuri medali za dhahabu kwa ushindi katika mbio za mita 200 wanawake na kuwaadhiri Marekani ambao kijadi ndio wenye kutamba kwenye fani hiyo ya riadha.

https://p.dw.com/p/F2fo
Shabiki akifurahia uhondo wa Michezo ya Olympik inayoendelea kupamba moto Beijing China.Picha: AP

Michezo ya Olympik huko Beijing

Wanarekani jana walikuwa na usiku wa jinamizi na kubwaga manyaga yao chini katika michuano yote miwili ya riadha wanawake na wanaume mbio za kupokezana mita 400.

Veronica Campbell- Brown wa kisiwa hicho cha Caribbean alijinyakulia medali ya dhahabu katika mbio za kasi mita 200 kwa kuongoza kwa mita moja.

Sura ya mshindi huyo wa mwaka 2004 ilikuwa ina mikunjo ya maumivu lakini ilikuja kutabasamu wakati alipomaliza mbio hizo ambapo alipiga magoti na kuomba mungu.

Bingwa wa dunia wa Marekani Allyson Felix alishika nafasi ya pili na mwanariadha anayeshikilia medali ya fedha mbio za mita 100 Kerron Stewart wa Jamaica alishika nafasi ya tatu.

Ushindi huo utazidi kuleta furaha kwa kisiwa hicho ambacho tayari kina kiwewe cha furaha kutokana na rekodi mbili za dunia na medali mbili za dhahabu za mbio fupi zilizonyakuliwa na mwanariadha wake Usain Bolt ambaye kasi yake imepongezwa mno na vyombo vya habari na wachambuzi wa michezo.

Jamaica pia imeshinda mbio za mita 100 wanawake.

Stewart amekaririwa akisema Wamarekani walihodhi mbio hizo hapo zamani lakini michezo hii ya Olympik imekuwa ni kwa ajili ya Jamaica.

Mkuu wa Kamati ya Olympik ya Kimataifa IOC Jacques Roge amehoji uwanamichezo wa Bolt wakati akisheherekea ushindi wake wa mita 100 hapo Jumamosi ambapo alikipiga kifua chake hata kabla ya kuvuka mstari wa kumalizia mbio hizo.

Roge amekaririwa akisema anafikiri mwanariadha huyo alikuwa akipaswa kuonyesha heshima zaidi kwa kupeana mikono na wenzake na kuwapongeza kwa kuwagonga begani sio kufanya ishara kama ile aliyoifanya.Amesema mwanariadha huyo inabidi apevuke.

Kocha wa Jamaica na mkimbiaji wa zamani wa mbio fupi Don Quarrie amemtetea Bolt kwa kusema kwamba kusheherekea kwake ushindi ni damu tu ya furaha za ujana kwa mtu ambaye ni mchangamfu,mwenye kufurahisha na mwenye furaha.

Marekani ilikuwa ikijishindia medali kuu ya dhahabu katika kila mbio fupi za michezo hiyo tokea mwaka 1984 na kujipatia medali za fedha na shaba mwaka huu kutakuwa faraja ndogo kwao.

Marekani imeshinda katika mbio za mita 400 wanaume abapo LeShawn Merritt alimshinda bingwa mtetezi wa mbio hizo Jeremy Wariner na kuwapatia Wamarekani medali ya saba ya dhahabu katika riadha.

Katika michuano mengine ya riadha bingwa mtetezi Yuri Borzakovysk wa Urusi,bingwa wa dunia wa mbio za ndani ya uwanja Abubakar Kaki wa Sudan na mwanariadha anayeshikilia medali ya fedha wa Afrika Kusini Mbulaeni Mulaudzi wote wameshindwa kuingia fainali za mbio za mita 800.

Licha ya Borzakovsyk kuwa katika hali nzuri msimu huu ameshindwa kujinowa kwa nusu fainali yake ya jana.Mrusi huyo alimalizia nafasi ya tatu ambapo wanariadha wawili tu husonga moja kwa moja katika fainali.

Kaki wa Sudan ameshindwa kabisa kwa kumalizia wa mwisho na Mlaudzi wa Afrika Kusini alimalizia wa sita na pia kutolewa katika fainali za hapo kesho.

Katika mojawapo ya michezo iliotia fora ni ushindi wa muogeleaji wa Uholanzi van der Weijden mwenye umri wa miaka 27 ambaye amelinganisha ushindi wake huo wa mita 10 na mapambano yake dhidi ya kansa ya damu miaka saba iliopita ambapo amesema inakufunza kuwa mwenye subira wakati unapokuwa umelazwa hospitalini na huo hasa ndio mkakakti alioutumia kuibuka na ushindi.

Mwanariadha wa Cuba Dyron Robles anayeshikilia rekodi ya dunia mbio za mita 110 kuruka viunzi ameshinda mbio hizo kiulaini lakini hakushangiliwa sana na mashabiki wa China kutokana na shujaa wao wa taifa Liu Xiang kujitowa katika mbio hizo kwa sababu ya majeruhi ya mguu.

Faraja nyengine kwa Marekani imekuja kutokana na ushindi wao wa bao moja bila ya majibu dhidi ya Brazil katika pambano la soka wanawake ambao umeimarisha hesabu yao ya medali na kutetea medali hiyo waliojinyakulia katika michezo ya Olympik ya Athens Ugiriki miaka minne iliopita.

Ilikuwa ni juhudi za kutia moyo zilizofanywa na Marekani ambao kwa muda mrefu walikuwa wakihimili shinikizo la Wabrazil wakiongozwa na washambuliaji hatari Marta na Christiane.

Goli la ushindi lilipatikana katika kipindi cha ziada ambapo mchezaji wa kiungo Carli Lloyd alithibitisha kuwa shujaa wa Marekani kwa bao lililomponyoka mlinda mlango wa Brazil Barbara katika dakika ya 96.

Mahasimu hao wawili walionyesha kabumbu safi kabisa lililojaa ushindani wa misuli na umahiri wa hali ya juu ambao umewachangasha watazamaji katika Uwanja wa Wafanyakazi mjini Beijing.

Wamarekani wanajijenga upya baada ya kampeni yao kali ya kuwania ubingwa wa dunia nchini China mwaka jana ambapo walifumuliwa na Brazil kwa mabao 4-0 katika nusu fainali na kuishia na medali ya shaba. Timu ya wanawake ya Ujerumani ilitwaa ubingwa huo wa soka wa dunia.

Ujerumani nayo imejishindia medali yake ya shaba ya tatu mfululizo katika michezo hiyo ya Olympik baada ya kuwabwaga Japani mabao 2 kwa nunge ushindi ambao umepatikana kwa taabu katika pambano la soka wanawake.

Timu ya mpira wa wavu wanawake ya Marekani imesonga mbele kuwania medali ya dhahabu baada ya kuishinda Cuba kwa seti tatu na kuwahakikishia Wamarekani hao nafasi bora ya Olympiki kuwahi kufikiwa katika mchezo huo tokea mwaka 1984.

Marekani itakutana na Brazil hapo kesho kuwania ubingwa huo wa Olympik.

Katika pambano dhidi ya Cuba hapo jana Marekani imeshinda kwa ponti 25-20,25-16 na 25-17. Marekani ilifikia nafasi hiyo baada ya kuzishinda China na Italia katika michuano ya robo fainali.

Brazili nayo pia imengia fainali baada ya ushindi wa seti tatu dhidi ya China.Cuba itapambana na China katika mechi ya kuwania medali ya shaba.

Na katika mchuano mkali kabisa uliowahi kuchezwa na wanawake wa Marekani katika michezo hiyo ya Olympik ya Beijing timu hiyo imewatoa Urusi kwa mabao 67-52 katika mechi ya mpira wa kikapu.

Sasa watakutana na Australia hapo kesho Jumamosi kuwania medali ya dhahabu baada ya Australia kuwawatoa China kwa mabao 90-56 katika mchezo mwengine wa nusu fainali.

Nayo timu ya mpira kikapu wanaume ya Marekani ambayo imewachenguwa mashabiki wa China inawekewa matumaini ya kuondoka na medali ya dhahabu walioikosa huko Athens leo inacheza na Argentina katika nusu fainali.

China inaendelea kuongoza kwa wingi wa medali ambazo ni 46 ikifuatiwa na Marekani yenye 29.

Katika michezo ya Olympik ya Athens ya mwaka 2004 itakumbukwa kuwa timu ya Marekani ilikuwa ikiongoza kwa medali nyingi ambazo zilikuwa 36 ikifuatiwa na China 32 ambayo ikiwa ni mwenyehi wa michezo hii ya Olympik inaelezwa kuwa imewekeza sana katika kuteuwa na kuwapatia mazoezi wanamichezo wake kwa miaka mingi.

Uingereza ina medali 17 na inashika nafasi ya 3 katika meza ya medali.Urusi inashika na nafasi ya 3 kwa kuwa na medali 16 wakati Australia imeshika nafasi ya 5 kwa kuwa na medali 11 ikifuatiwa na Ujerumani ambayo pia ina medali 11.