1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Wajerumani hawajuani"

Maja Dreyer3 Oktoba 2007

Na bila shaka, wahariri wa hapa nchini hawawezi kukosa suala muhimu la leo ikiwa ni siku ya kusherehekea muungano wa Ujerumani. Vipi basi, magazeti ya kutoka Mashariki na Magharibi yanachunguza hali ya muungano?

https://p.dw.com/p/CHRh
Watu waliopanda ukuta wa Berlin hapo Novemba 1989
Watu waliopanda ukuta wa Berlin hapo Novemba 1989Picha: AP

Gazeti la “Nordwest-Zeitung” kutoka Magharibi mwa Ujerumani ambalo linakumbusha siku za muungano:

“Ni picha za kufurahia kweli: Watu waliopanda juu ya ukuta katikati mwa Berlin, raia wa Ujerumani Mashariki ambao walivuka mpaka uliofunguliwa, na pia sherehe za muungano hapo Oktoba 3 mwaka 1990 huko Berlin. Hata miaka 17 baada ya hapo ni vizuri kukumbuka matukio haya. Lakini kwa nini bado hakuna kumbukumbu ya muungano katika mji mkuu?”

Mhariri wa “Westfalenpost” anachambua maendeleo tangu muungano na ameandika:

“Kweli, mengi yalifikiwa. Tunaweza kujivunia licha ya matatizo yaliyopo. Ukiangalia miji ya Leipzig, Dresden au Berlin huwezi kusema kuna tofauti ya kiuchumi. Lakini tusisahau kuwa baada ya miaka 17 bado watu wengi hususan vijana wenye elimu nzuri wanakimbia upande wa Magharibi kutafuta kazi.”

Gazeti la “Thüringer Landeszeitung” la upande wa Mashariki linatathmini umoja kati ya wananchi likiandika:

“Kinachosikitisha kwenye siku hii ya kuadhimisha muungano kati ya raia wa Ujerumani Mashariki na Magharibi ni kwamba watu hawajuani. Je, nani anajua maisha kwenye upande mwingine yalikuaje? Ikiwa tutaendelea kuwatilia dhana watu wa upande mwingine tutakuwa na bonde kubwa zaidi.”

Na hatimaye kuhusu suala hilo ni mhariri wa “Mittelbayerische Zeitung” ambaye anataka serikali iongeze juhudi zake za kuleta umoja. Ameandika:

“Ukiangalia vile makundi ya kisiasa yenye msimamo mkali, uwe ni wa mrengo wa kushoto au wa kulia, kweli inafaa kubadilisha sera. Kansela Merkel anapaswa kulishughulikia mwenyewe ujenzi wa sehemu ya Mashariki. Nani isipokuwa yeye kama mzaliwa wa Mashariki anafaa zaidi kwa kazi hiyo?”

Naam, juu ya sherehe hapa nchini kuna mada nyingine za kimataifa ambazo zinazingatiwa na wahariri wa magazeti. Gazeti la “Mitteldeutsche Zeitung” linajihusisha na mkutano kati ya viongozi wa Korea Kusini na Kaskazini hapo jana na limechambua:

“Hali inatulia na matumaini ya sehemu hizo mbili za Korea kuungana yanaongezeka. Lakini haya yatachukua muda, kwani nchi hizo mbili zilielekea njia tofauti za kisiasa na kiitikadi. Kuiangusha seng'enge pekee hakutaleta muungano. Kazi itakuwa ngumu kuliko katika nchi nyingine katika historia.”

Matokeo huko Myanmar na ziara ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Ibrahim Gambari pia linatathminiwa na wahariri. Huyu hapa ni mhariri wa “Nürnberger Zeitung” ambaye ameandika:
“Ibrahim Gambari angepaswa zaidi asafiri China ambao ina usemi mkubwa badala ya kuwafuata viongozi wa Myanmar kwenye mji mkuu wao uliko msituni. China inategemea mali ghafi za Myanmar na Myanmar inategemea kupata silaha kutoka China na kuuza bidhaa zao kwenye soko la China. Huenda kutisha kuisusia michezo ya Olympiki huko China mwakani kutahamasisha serikali huko Beijing kubadilisha msimamo wake juu ya suala la Myanmar.