1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wapiga kura kulichagua bunge

Sekione Kitojo
24 Septemba 2017

Leo tarehe 24 Septemba ,Wajerumani wanapiga kura katika uchaguzi mkuu, ambapo kiongozi wa chama cha Christian Democratic -CDU Kansela Angela Merkel anawania kuchaguliwa tena kwa muhula wa nne wa kipindi cha miaka minne.

https://p.dw.com/p/2kaLV
Berlin Bundestagswahl Stimmzettel und Wahlurne
Picha: Reuters/S. Loos

Mpinzani wake mkubwa  wa kiti cha Ukansela ni mkuu wa chama cha Social Democratic SPD, ambacho hadi uchaguzi huu kilikuwa mshirika katika serikali ya Muungano pamoja na CDU.

Wajerumani wanapiga  kura leo Jumapili  katika  uchaguzi ambao unatarajiwa  kushuhudia  kansela  Angela  Merkel akishinda muhula  wa  nne wa  kihistoria  na  chama  cha siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  kikitarajiwa  pia  kuingia bungeni kwa  mara  ya  kwanza  katika  muda  wa  zaidi ya nusu  karne.

Deutschland Wahlkabine Europa- und Kommunalwahl
Wajerumani wakipiga kura katika uchaguzi mkuu wa taifa kulichagua bungePicha: picture alliance/dpa

Kundi  la  kihafidhina  la  kansela  Merkel  linaelekea kubaikia  kuwa  kundi  kubwa  bungeni , uchunguzi  wa maoni  ya  wapiga  kura umeonesha  kabla  ya  kura hiyo leo, lakini  mgawanyo  wa  wa  makundi  ya  kisiasa utamuwia  vigumu  kuunda  serikali  ya  mseto  kuliko  hapo nyuma.

Wakati karibu  theluthi  ya  Wajerumani  hawajaamua wachague  chama  gani  wakati  wa  kuelekea  upigaji kura, Merkel  na  hasimu  wake  mkubwa katika kinyang'anyiro  hiki, mgombea  wa  chama  cha  siasa  za wastani  za  mrengo  wa  kushoto Martin Schulz wa  chama cha  Social Democratic SPD, amewahimiza  wapiga  kura jana  Jumamosi  kujitokeza  na  kupiga  kura.

"Tunataka  kuwapa  hamasa  zaidi  ili  tuweze kuwafikia watu  wengi  zaidi ," kansela mwenye  umri  wa  miaka  63, alisema  mjini  Berlin  kabla ya  kuelekea  kaskazini  katika jimbo  lake  kwa  ajili  ya  duru  ya  mwisho  ya  kampeni.

Uchaguzi wa majimbo pigo kwa Merkel

Deutschland Wahlkampf CSU/CDU auf dem Marienplatz in München
Baadhi ya vipeperushi dhidi ya kansela Maerkel mjini Berlin, kikieleza kuwa "huyu sie kansela wangu".Picha: picture alliance/dpa/S. Hoppe

Katika uchaguzi  wa  majimbo  mwaka  jana, chama  cha kansela  Merkel cha  kihafidhina  kilipata  pigo dhidi  ya chama  cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia  cha Alternative for Germany AfD , chama  mbadala  kwa Ujerumani, ambacho  kilifaidika  na hali ya  wapiga  kura kutoridhishwa na uamuzi  wake  kuweka  mipaka  ya Ujerumani  wazi kwa  ajili  ya  wahamiaji  milioni  moja.

Hali  hiyo ya kushindwa ilimfanya  Merkel , ambae  ni  binti wa mchungaji  ambaye  alikulia  katika  Ujerumani  ya mashariki  ya  kikomunist, kufikiria iwapo ajaribu  kugombea kuchaguliwa  tena.

Lakini  baada  ya  suala  hilo  la  wakimbizi  kulidhibiti mwaka  huu, alirejea  tena  katika  umaarufu  na  kujitupa tena  kufanya  kampeni , akijiwakilisha  kuwa  ni mhimili  wa uthabiti  katika  dunia  ambayo  haina  uhakika.

Chama cha  siasa kali za mengo wa kulia

Kiongozi wa chama  cha  siasa kali za  mrengo wa kulia Alexander Gauland, muasisi mwenza na naibu mwenyekiti wa  chama  hicho  cha  AfD amesema "tutairejesha  nchi yetu kwenu kwa  kuzuwia mmiminiko  wa  wakimbizi." Katika  suala  la  kuunda  serikali  ya  mseto  ambapo vyama vya muda  mrefu SPD, na CDU vimesema havitafikiria  kuungana  na  chama  hicho  kuunda  serikali, kiongozi wa  chama  cha  AfD Gauland  amesema "hatutaingia  katika  muungano na chochote  kati  ya vyama  hivyo pia. Tutabakia  kuwa chama  cha  upinzani tukiwa na msimamo  thabiti."

"Schlussrunde" von ARD und ZDF zur Bundestagswahl | Alexander Gauland
Kiongozi wa chama cha Alternative for Germany AfD Alexander GaulandPicha: picture alliance / Maurizio Gambarini/dpa

Uchaguzi  wa  leo  wa  taifa  nchini  Ujerumani  utaashiria mwanzo wa  mjadala  mpya  hata  hivyo  katika  kuweka sawa  mapungufu  kuhusiana  na sarafu  ya  pamoja  ya euro.

Rais  wa  Ufaransa Emmanuel Macron ameweka  wazi kwamba  anapendelea  kusukuma  mageuzi  ili  kuimarisha sarafu  ya  euro  na  anatarajiwa  kutoa  mapendekezo katika  hotuba  yake  muhimu siku  ya  Jumanne.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / ape