1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani watatu, watekwa na waasi wa Kikurd.

Nyanza, Halima10 Julai 2008

Jeshi la Uturuki, linawatafuta wapanda milima watatu wa Kijerumani waliokamatwa na waasi wa Kikurd nchini humo.

https://p.dw.com/p/EZmF
Mlima Ararat ulioko mpakani mwa Uturiki na Armenia, ambapo Wapanda milima watatu wa Kijerumani, walitekwa Jumanne na waasi wa Kikurd .Picha: AP

Wapanda milima hao watatu, ni sehemu ya timu ya wapandamilima wa Kijerumani 13 waliokamatwa katika kambi yao, wakati wakipanda mlima Ararat mashariki mwa Uturuki Jumanne wiki hii.

Kikosi hicho cha jeshi, kimekuwa kikifanya operesheni katika jimbo hilo la Agri kuweza kuwapata Wajerumani hao watatu.

Msaidizi wa Gavana wa Jimbo hilo, Camel Kaya amesema matumaini yao ni kwamba wataachiliwa huru na bila ya madhara yoyote.

Mpaka sasa bado haijulikani walipo mateka hao, ambapo wenzao 10 walionusurika kutekwa pamoja na walinzi wao, tayari wamerudi katika mji wa Dogabeyezit, katika jimbo la Agri nchini humo, kutoka katika eneo hilo la milima ambako wenzao hao walitekwa nyara na waasi wapatao watano.

Gavana wa jimbo hilo la Agri, amesema bado wanaendelea na juhudi kuweza kuwapata mateka hao.

Wapanda milima hao wote waliotekwa nyara, wanatokea katika mkoa wa Bavaria hapa Ujerumani.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa mkoa wa Bavaria Joachim Hermann, kambi ya timu hiyo ya wapanda milima hao 13 ilivamiwa katika mlima Ararat mpakani na Armenia.

Kufuatia kutekwa kwa Wajerumani hao na waasi wa Kikurd wa PKK Jumanne usiku, serikali ya Uturuki imefunga shughuli zote za upandaji wa mlima huo wa Ararat.

Gavana wa jimbo hilo la Agri, Metin Cetin amesema shughuli za upandaji mlima huo zimesitishwa mpaka pale taarifa zitakapotolewa tena, ili kupisha operesheni inayoendelea kuwatafuta wapanda milima hao.

Katika miaka ya hivi karibuni Ujerumani imekuwa ikishirikiana na serikali ya Uturuki kujaribu kusimamisha shughuli za waasi hao wa PKK hapa nchini.

Ni mwezi uliopita tu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble, alipiga marufuku matangazo yaliyokuwa yakifanywa na kituo kimoja cha televisheni, ambacho Uturuki ilikuwa ikikilaumu kwa kufanyia propaganda waasi hao wa PKK.

Aidha Ujerumani pia imekuwa mstari wa mbele kuwarudisha Uturuki, raia wa Kituruki wanaoishi nchini humu, ambao wanashukiwa kuwa ni wanachama wa kundi hilo la waasi.

Kwa mujibu wa Gavana wa jimbo hilo la Agri walikokamatwa wapanda milima hao, hatua ya waasi hao, kuwateka watu hao ni kupinga serikali ya Ujerumani inavyochukua hatua dhidi ya kundi hilo la waasi.

Wakati huo huo Waasi hao wa kundi la PKK leo wanatarajia kutoa taarifa kuhusiana na suala hilo.