1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wauawa katika shambulizi Uturuki

12 Januari 2016

Serikali ya Uturuki, imesema kiasi ya raia tisa wa Ujerumani ni miongoni mwa watu walioawa katika shambulizi la bomu la kujitoa muhanga lililotokea kwenye eneo la kitalii mjini Istanbul.

https://p.dw.com/p/1Hc1m
Picha: Reuters/O. Orsal

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu amemwambia Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kuwa watu tisa kati ya 10 waliouawa katika shambulizi hilo ni raia wa Ujerumani.

Hayo ameyaeleza katika mazungumzo yao kwa njia ya Simu. Davutoglu ametuma salamu za rambirambi kwa Merkel na amemuhakikishia kuwa taarifa zaidi kuhusu uchunguzi unaoendelea wa shambulizi hilo la kujitoa muhanga zitatolewa kwa maafisa wa Ujerumani. Amesema shambulizi hilo linaonekana kufanywa na kundi lenye itikadi la Dola la Kiislamu-IS.

Akizungumza awali mjini Berlin, Kansela Merkel alisema huenda Wajerumani ni miongoni mwa watu waliouawa. Taarifa hizo pia zilielezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Merkel amesema baadhi ya watu waliokuwemo kwenye kundi la utalii la Ujerumani ni miongoni mwa wahanga na kwamba maafisa wa Ujerumani wanashirikiana na wenzao wa Uturuki kubaini zaidi uraia wa wahanga hao.

Ahmet Davutoglu akiwa na Angela Merkel
Ahmet Davutoglu akiwa na Angela MerkelPicha: picture-alliance/AA/H. Goktepe

Akizungumza mjini Ankara, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amelaani vikali shambulizi hilo la kigaidi. ''Kwa bahati mbaya tumewapoteza watu 10. Tutaendelea kuwatangazia kadri tunavyoendelea na uchunguzi wetu. Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi wale wote waliopoteza maisha yao na ninawaombea waliojeruhiwa wapone haraka,'' alisema Erdogan.

Ujerumani yawasihi raia wake kutozuru maeneo ya kitalii

Muda mfupi baada ya shambulizi hilo kutokea, Ujerumani iliwaonya raia wake kuepuka kutembelea maeneo ya kitalii ya mji wa Istanbul, wenye watu milioni 14 na ambao umekuwa na mashambulizi kadhaa yaliyosababisha mauaji.

Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki, Numan Kurtulmus amesema watu wengine 15 wamejeruhiwa huku wawili wakiwa katika hali mbaya. Hata hivyo bado haijafahamika iwapo katika watu waliouawa, yumo pia mshambuliaji aliyejitoa muhanga, ambaye ni raia wa Syria mwenye umri wa miaka 28.

Waziri Mkuu wa Algeria, Abdelmalek Sellal amesema kuna umuhimu wa kuendelea na mapambano dhidi ya ugaidi katika njia zote na kwamba nchi yake itapambana na kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS, ili kuhakikisha usalama thabiti.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na Kansela Merkel wakati wa ziara yake mjini Berlin, Sellal ametoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu shambulizi la leo la Istanbul, ambalo limelaaniwa vikali pia na muungano wa upinzani wa Syria.

Raia wa Ujerumani wakiondoka Istanbul baada ya shambulizi
Raia wa Ujerumani wakiondoka Istanbul baada ya shambuliziPicha: picture-alliance/epa/C. Turkel

Picha zinaonyesha miili ya watu kadhaa ikiwa imekatika karibu na msikiti maarufu wa buluu wa enzi za utawala wa Ottoman katika uwanja wa Sultanahmet, kwenye wilaya ambayo ina alama za minara ya kihistoria kwenye mji wa Istanbul.

Shirika la habari la Uturuki, Dogan, limeripoti kuwa raia tisa wa Ujerumani na wawili wa Peru ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa. Pia wako raia kutoka Norway na Korea Kusini. Majeruhi hao wanapatiwa matibabu katika hospitali za mji huo.

Taarifa zinaeleza kuwa Davutoglu ameitisha mkutano wa dharura kuhusu usalama na mawaziri muhimu pamoja na maafisa waandamizi wa Uturuki, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, Efkan Ala na mkuu wa shirika la upelelezi la nchi hiyo, Hakan Fidan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman