1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani wahisi wako salama licha ya matukio ya ugaidi

Isaac Gamba
6 Januari 2017

Utafiti wa maoni  uliofanywa  unaonyesha kuwa watu wengi nchini Ujerumani  wanahisi wako salama licha ya shambulizi la hivi karibuni la mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/2VNy4
Deutschland Berlin - Polizei patroulliert am wieder geöffneten Weihnachtsmarkt am Breitscheidplatz
Picha: Reuters/F. Bensch

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na kituo cha matangazo ya umma cha ARD na gazeti moja nchini humo la Die Welt mwanzoni mwa mwaka huu ikiwa ni wiki mbili baada ya kufanyika shambulizi la mjini Berlin asilimia 73 ya wale waliohojiwa wanajiona kuwa salama wakati asilimia 26 wanahisi kutokuwa salama. Watu 12 waliuawa na wengine 50 walijerhiwa wakati mshambuliaji alipoendesha lori katika soko la Krismasi lililokuwa limejaa watu mjini Berlin. Kwa ujumla matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa wananchi wengi nchini Ujerumani wanaona wako salama tofauti na jinsi wanavyofikiria wanasiasa.

Aidha kwa mujibu wa utafiti huo wa maoni kiwango cha ufuatiliaji wa watu au vitu vinavyotiliwa mashaka kiusalama nacho pia kinaonekana kupungua. Licha ya ukosoaji wa hivi karibuni dhidi ya vyombo vya usalama kufuatia mashambulizi ya mjini Berlin bado raia wengi wa Ujerumani wanaona wako salama.

Kufuatia vitendo vya udhalilishaji kingono katika mji wa Cologne na miji mingine mwaka jana, vyombo vya usalama nchini Ujerumani vimekuwa vikikosolewa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake barabara. Hata hivyo imani ya watu juu ya jeshi la polisi nchini Ujerumani sasa inaonekana kuongezeka ambapo asilimia 88 ya watu wanaonekana kuwa na imani na jeshi hilo.

Imani juu ya taasisi za kijasusi yapungua

Deutschland LKW nach dem Anschlag am Breitscheidplatz in Berlin
Lori lililohusika katika shambulizi mjini BerlinPicha: Reuters/H. Hanschke

Zaidi ya nusu ya watu waliohojiwa katika utafiti huo wa maoni wameonesha kuwa na imani ndogo au kutokuwa na imani kabisa na taasisi zinazohusika na masuala ya ujasusi wa ndani na nje za Ujerumani.

Suala la usalama wa ndani na hatua dhidi ya vitisho vya ugaidi ni masuala muhimu ambayo wapiga kura nchini Ujerumani wangependelea yazingatiwe. Asilimia 11 ya waliohojiwa katika utafiti huo wanasema wangependelea masuala hayo kuwa kipaumbele cha serikali.

Suala ambalo limepewa umuhimu wa kwanza na watu wengi waliohojiwa ni suala linalohusiana na mgogoro wa wakimbizi ambapo asilimia 40 wanashauri lingepewa kipaumbele. Aidha kumekuwa na ongezeko kidogo kwa kiwango cha asilimia tatu kuhusiana na hofu ya watu kiusalama.

Ukilinganisha na mwezi Disemba mwaka jana, hisia za kisiasa zinaelekea zaidi upande wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU na mshirika wake chama cha Christian Social Union, CSU pamoja na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany, AfD ambavyo vimejiongezea asilimia mbili ya uungwaji mkono kutokana  na utafiti uliofanywa ukihusisha swali lililopewa jina la "Swali la Jumapili" lililohoji "chama kipi utakipigia kura iwapo uchaguzi ungefanyika Jumapili?"

Kwa upande mwingine chama cha cha Social Democrats, SPD na chama cha kijani umaarufu wake umeonekana kupungua kufuatia utafiti huo wa maoni. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo sasa muungano mwingine unaofahamika kama  "Muungano Mkuu" kati ya SPD kilicho na asilimia 20 na CDU/CSU vyenye asilimia 37 unawezekana.

Mwandishi: Isaac Gamba/DW/DPA

Mhariri: Grace Patricia Kabogo