1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa COP28 wahangaikia kufikia makubaliano

12 Desemba 2023

Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika Dubai, umeingia katika muda wa ziada huku washiriki wakihangaika kukubaliana juu ya rasimu ya mwisho ya makubaliano.

https://p.dw.com/p/4a3aY
UN-Klimakonferenz in Dubai 2023 | COP 28 | Protest
Wanaharakati wa mazingira waandamana wakati wa mkutano wa COP28 huko Dubai.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika Dubai, umeingia katika muda wa ziada huku washiriki wakihangaika kukubaliana juu ya rasimu ya mwisho ya makubaliano.  

Soma pia: Katibu Mkuu wa UN Gutteres ahimiza makubaliano COP28

Mkutano huo ulitarajiwa kumalizika leo Jumanne saa tano asubuhi lakini matumaini ya kufikia makubaliano kwa wakati uliopangwa yamefifia.  Wawakilishi kutoka nchi 200 wanaendelea kujadili rasimu ya mpango wa mazingira ambayo kufikia sasa suala la kuondoa nishati ya visukuku linaendelea kuibua mvutano.

Mnamo Jumatatu jioni, rais wa COP28, Sultan Al Jaber, alisambaza rasimu yenye kurasa 21 inayodhamiria kusaka muafaka kati ya mataifa yapatayo 200, ikiwemo Saudi Arabia na mataifa mengine yanayozalisha mafuta kwa wingi, juu ya upunguzaji wa hewa chafu lakini pia kuzuwia kusambaratika kwa chumi za mataifa hayo.

Rasimu hiyo imeibua shutuma kali kutoka kwa Marekani, Umoja wa Ulaya, mataifa yenye mazingira magumu na wataalam wa mazingira.

Mjumbe wa mabadiliko ya tabianchi wa Marekani, John Kerry, aliwaambia mawaziri kwamba mkutano huo ndio wa mwisho kuweza kupata fursa ya kuifanya dunia kuwa salama.

Soma pia: Guterres ahimiza makubaliano ya kuachana na nishati za visukuku

Makubaliano ya mazingira yalielezea mikakati kadhaa ambayo nchi zinaweza kuchukua kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, lakini iliacha mahitaji muhimu kutoka kwa mataifa mengi hasa linapokuja suala la kuachana na matumizi ya nishati ya visukuku.

Upinzani wa matumizi ya mafuta

U.N.-Klimagipfel COP28 in Dubai
Rais wa COP28 Sultan al-Jaber katika mkutano wa COP28 huko Dubai.Picha: Peter Dejong/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na China na wazalishaji wakuu wa mafuta kama Saudi Arabia, zimeripotiwa kupinga makubaliano ambayo yanayotazamia mwisho wa matumizi ya mafuta.

Wawakilishi kutoka mataifa ya Visiwa vya Pasifiki ya Samoa na Visiwa vya Marshall, ambao tayari wameshuhudia athari za kuongezeka kwa bahari, wameitaja rasimu hio kama "waraka wa kifo."

Akizungumza na waandishi wa habari waziri wa Mazingira wa Samoa Cedric Schuster amesema hawawezi kusaini maandishi ambayo hayana dhamira thabiti ya kukomesha matumizi ya nishati ya visukuku.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu, wa mkurano huo Balozi Majid Al-Suwaidi, amesema urais wa COP28 unataka mafuta ya visukuku yatajwe kwa maandishi:

"Tumejua kwa muda mrefu kwamba lugha inayozungumzia nishati ya visukuku ni ngumu, na maoni yake ni magumu, ni muhimu kuwa na lugha sahihi linapokuja suala la nishati. muhimu tufikirie jinsi gani tunapata  uwiano, wapo wanaotaka iondolewe kwa awamu, wapo wanaotaka ipunguzwe kwa awamu, wapo wanaotaka hatua tofauti. Jambo muhimu ni kupata maridhiano. Na hatutaki muelekuo mmoja ambao utasababisha vikwazo katika mchakato. Tunahitaji wahusika kuja pamoja kwa sababu tunahitaji kufikia lengo."

Wakati huo huo, Rais wa COP28, Sultan Al Jaber, ametoa wito kwa mataifa katika mkutano huo kuongeza juhudi zao kufikia makubaliano kabla ya muda wa mwisho uliopangwa wa mkutano huo.