1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa ECOWAS watarejea Cote d'Ivoire

29 Desemba 2010

Viongozi wa Afrika Magharibi wamekiri kuwa walishindwa kusuluhisha mzozo wa kisiasa wa Cote d'Ivoire walipokutana na Laurent Gbagbo mjini Abidjan hiyo jana.Kwa hivyo,wiki ijayo watarejea huko kwa mazungumzo zaidi.

https://p.dw.com/p/Ql5y

Siku ya Jumanne, viongozi hao walishindwa kumshawishi Laurent Gbagbo kuondoka madarakani licha ya tishio la kutumiwa nguvu za kijeshi. Marais wa Benin,Sierra Leone na Cape Verde wamekabidhiwa na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS- jukumu la kuumaliza mzozo wa Cote d'Ivoire, baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita kusababisha mapambano kati ya wafuasi wa Gbagbo na wa mpinzani wake, Alassane Ouattara, anaetambuliwa kimataifa.

Leo, marais hao watatu walikutana na mwenyekiti wa ECOWAS, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, mjini Abuja, baada ya hiyo jana kutofanikiwa kumshawishi Gbagbo kuondoka madarakani kwa hiyari licha ya tishio la kukabiliwa na nguvu za kijeshi.

Baada ya mkutano wa leo hii, Rais Jonathan alisema wajumbe hao watatu watarejea Cote d'Ivoire Januari 3 kuendelea na majadiliano yao pamoja na Gbagbo. Matokeo ya ziara hiyo ya pili ndio yatakayoamua hatua ya kuchukuliwa. Kwa mujibu wa afisa mmoja katika wizara ya mambo ya nje ya Cape Verde, hapo awali, Laurent Gbagbo alipewa muda wa saa 24 kuzingatia ujumbe aliokabidhiwa, lakini aliomba kupewa muda hadi wiki ijayo.

Bildausschnitt von Jonathan Goodluck. French Prime Minister Francois Fillon, left, stands with Nigerian d Vice President Goodluck Jonathan as he meets for talks with leaders of Africa's most populous nation, at the Presidential Villa in Abuja, Nigeria Friday, May 22, 2009. Fillon later told reporters that France was Nigeria's second-largest investor after the United States, and he praised Nigeria for contributing to peacekeeping missions across Africa. (AP Photo/Abayomi Adeshida)
Mwenyekiti wa ECOWAS, Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.Picha: AP

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria, kama kiongozi wa nchi iliyo imara kijeshi na kiuchumi katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi, anatazamiwa kutoa mwongozo iwapo nguvu za kijeshi zitumiwe. Mataifa makuu na majirani wa Kiafrika katika kanda hiyo wanamshinikiza Gbagbo kumkabidhi madaraka mpinzani wake, Ouattara, kufuatia uchaguzi wa utata uliofanyika Novemba 28.

Uchaguzi huo uliazimia kuleta umoja kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002 hadi 2003 katika nchi iliyo mzalishaji mkubwa kabisa wa kakao duniani. Matokeo yaliyotangazwa na tume ya Uchaguzi yalionyesha kuwa Ouattara aliongoza kwa asilimia 8, lakini mahakama kuu ya kikatiba inayoongozwa na mshirika wa Gbagbo kwa haraka ilibatilisha matokeo hayo kwa madai kuwa kulifanyika udanganyifu. Wote, Gbagbo na Ouattara, wanadai kushinda uchaguzi huo, lakini Ouatttara ndio anaetambuliwa kama rais na jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na ECOWAS na Umoja wa Mataifa. Wakati huo huo, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeweka vikwazo dhidi ya Gbagbo na washirika wake wa karibu. Kwa upande mwingine, Benki ya Dunia na Benki Kuu ya kanda ya Afrika Magharibi zimesita kutoa fedha kwa kiongozi huyo wa Cote d'Ivoire katika jitahada ya kumdhoofisha madarakani.

Mwandishi:P.Martin/RTRE/AFPE

Mpitiaji:Othman, Miraji