1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa OSCE washikiliwa na waasi

Abdu Said Mtullya29 Mei 2014

Rais Mteule wa Ukraine Poroshenko amethibitishwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais,wakati kiongozi wa waasi wa mashariki mwa Ukraine amesema wapiganaji wake wanawashikilia wajumbe wa OSCE

https://p.dw.com/p/1C8rJ
Petro Poroshenko athibitishwa kuwa mshindi
Petro Poroshenko athibitishwa kuwa mshindiPicha: Reuters

Aliejitangaza kuwa Meya wa umma wa mji wa Slovyansk katika jimbo la Donetsk ,Vyacheslav Ponomarev ameliambia shirika la habari la AP kuwa wajumbe hao wanne, kutoka Uturuki,Uswisi,Estonia na Denmark wamo katika mikono ya wapiganaji wake na kwamba wapo katika hali salama.

Kiongozi huyo wa waasi amesema alilitahadharisha Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya,OSCE juu ya kutowapeleka wajumbe wake katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi lakini amesema maafisa hao waliingia katika sehemu hizo licha ya tahadhari iliyotolewa. Hata hivyo ameahidi kwamba wajumbe hao wataachiwa baada ya mkasa wao kushughulikiwa ingawa hakusema ni lini.

Shirika la OSCE liliarifu Jumatatu iliyopita kuwa liliyapoteza mawasiliano na afisa wake mmoja aliekuwamo katika ujumbe wa watu wanne katika jimbo la Donetsk. Wanaharakati wanaoegemea Urusi hapo awali waliwahi kuwateka nyara wajumbe wa kijeshi wanaofanya kazi chini ya udhamini wa shirika la OSCE.

Wajumbe wa shirika hilo wamepelekwa nchini Ukraine ili kuifuatilia hali ya usalama nchini humo baada ya Urusi kulichukua jimbo la Krimea na kuliingiza katika sehemu yake. Shirika la OSCE linataka wafanyakazi wake waachiwe mara moja na bila ya masharti yoyote. Mwenyekiti wake Didier Burkhalter amesema mkasa wa kushikiliwa wajumbe wa shirika lake na waasi wa mashariki mwa Ukraine utazitatiza juhudi za kuutatua mgogoro wa nchini Ukraine.Bwana Burkhalter amesema kadhia kama hizo haziwezi kuvumiliwa.

Poroshenko athibitishwa mshindi wa uchaguzi

Wakati huo huo Rais Mteule wa Ukraine Petro Poroshenko leo amethibitishwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.Rais wa kipindi cha mpito Oleksander Turchynov ameliambia Bunge la Ukraine kwamba Poroshenko ameshinda kwa kupata asilimia 54 .7 ya kura.

Turchynov amesema matayarisho yote yanafanyika kwa ajili ya sherehe za kumwapisha Poroshenko katika muda wa siku 15 zijazo.

Majeshi ya serikali yapata pigo

Lakini katika upande mwingine majeshi ya serikali ya Ukraine yamepa pigo jingine baada ya waasi kufanya shambulio mashariki mwa Ukraine.Watu waliokuwa na silaha waliivamia kambi ya jeshi katika jimbo la Lugansk karibu na Urusi. Shambulio hilo limefanyika siku moja baada ya majeshi ya serikali ya Ukraine kuudhibiti tena uwanja wa ndege wa kimataifa katika jimbo la Donetsk uliokuwa unashikiliwa na waasi.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afpe

Mhariri: Josephat Charo