1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa Umoja wa Mataifa wako Afrika kuhimiza amani

Mohamed Dahman1 Juni 2008

Wanadiplomasia wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wako ziarani barani Afrika kushinikiza amani na demokrasia.

https://p.dw.com/p/EAhl
Wakimbizi kutoka jimbo la Darfur nchini Sudan waliokimbiilia Chad wakimbizi hao ni sehemu ya watu milioni mbili na nusu walipotezewa makaazi yao kutokana na mzozo wa Dafur.Picha: AP

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanawasili mjini Nairobi Kenya leo hii kuanza ziara ya nchi sita barani Afrika kuendeleza amani huko Dafur Sudan,Somalia na mashariki mwa Congo na kujaribu kuzuwiya vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali ya Sudan na waasi wa zamani wa kusini mwa nchi hiyo.

Wakati wa ziara yao ya siku tisa barani humo wanadiplomasia wa baraza hilo watakutana na wahusika wengi wakuu katika maeneo ya migogoro barani Afrika na kuzungumza na watu wachache miongoni mwa mamilioni ya wale waliopotezewa makaazi kutokana na mzozo wa miaka mitano wa Dafur ambao umeenea hadi Chad na pia wale wa mzozo wa mashariki ya Congo.

Chombo hicho chenye madaraka makubwa cha Umoja wa Mataifa ammbacho kinawajibika na suala la kudumisha amani na usalama wa kimataifa pia kitashajiisha demokrasia dhaifu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi mpya halikadhalika Ivory Coast ilioibuka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe hivi karibuni na ambayo inafanya uchaguzi wake wa rais hapo tarehe 30 mwezi wa Novemba.