1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa kusini mwa Sudan wanatumai nchi yao itaungana

Josephat Charo29 Januari 2008

Kura ya maoni kufanyika mwaka wa 2011

https://p.dw.com/p/Cz0M
Rais wa Sudan Omar el Bashir (kushoto)Picha: AP

Wakaazi wa eneo la kusini mwa Sudan, ambao kwa muda mrefu wamejikuta katika vita vya madaraka na eneo la kaskazini linalodhibitiwa na serikali, wanasubiri kwa hamu kubwa wakiwa na matumaini lakini wakati huo huo wakiwa na wasiwasi wakati watakapopiga kura ya moani mwaka wa 2011 kuamua ikiwa eneo la kusini litaendelea kubakia sehemu ya Sudan.

Baadhi ya wakaazi wa kusini mwa Sudan wana matumaini Sudan itaungana na kuwa nchi moja.

Kura za maoni zitafanyika sambamba katika maeneo ya milima ya Nuba, Blue Nile na Abyei kuamua ikiwa maeneo hayo yatakuwa sehemu ya Sudan kusini au Sudan. Mizozo kati ya serikali ya Sudan na makundi ya waasi katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo imeifanya nchi hiyo kuwa nyumbani kwa idadi kubwa ya watu duniani waliolazimika kuyahama makazi yao wakiwa nchini mwao.

Takwimu zinaonyesha watu milioni sita wamelazimika kuzikimbia nyumba zao wakiwemo wakaazi wa maeneo ya Nuba, mashariki mwa Sudan na jimbo la Darfur.

Kwa sababu ya ukosefu wa uzoefu, ufisadi na uamuzi wa jumuiya ya kimataifa kuushughulikia zaidi mzozo wa Darfur, Sudan Kusini kwa kasi ya kinyonga imekuwa ikijenga miundombinu thabiti baada ya serikali yake kuundwa kufuatia miaka 50 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka wa 2005.

Wakaazi wa kusini mwa Sudan waliokwenda kuishi katika eneo la kaskazini, hususan katika mji mkuu Khartoum, wanasema wanataka umoja wa nchi yao. Lakini pia wanasema umoja huo utategemea ikiwa serikali ya Sudan itatekeleza makubaliano ya mkataba wa amani uliosainiwa kati yake na waasi wa zamani wa kundi la Sudan People´s Liberation Movement, SPLM.

Moja kati ya makubalino ya mkataba huo ni kura hiyo ya maoni, pamoja na kuendeleza utawala wa kidemokrasia nchini kote na kugawana faida inayotokana na uuzaji wa mafuta.

´Mkataba wa amani ulimfurahisha kila mtu, hasa katika eneo la kusini, ´amesema Charles Wani Ladu, mwandishi wa habari wa gazeti la Monitor mjini Khartoum, aliyeiacha nyumba yake kusini mwa Sudan kwenda kusoma elimu ya mawasiliano ya umma katika chuo kikuu cha Juba.

Mwandishi huyo wa habari anasema mkataba huo wa amani umeleta mabadiliko mengi mazuri na kubadili hisia za watu. Watu wengi waliteseka sana kimawazo lakini sasa wana amani.

Hii inataoa nafasi kwa umoja kupatikana. Wakaazi wa kusini mwa Sudan walianzisha vita kupinga hatua ya serikali ya Khartoum kuwatenga na kutoyashughulikia masilahi yao.

Baada ya mkataba wa amani kusainiwa lazima kuwepo haki ya huduma na nafasi za ajira na pia usawa wa kila kitu. ´Sudan iliyoungana inaweza kupatikana. Viongozi wanaweza kulifikia hilo,´ amesema Charles Wani Ladu.

Akizungumzia kura ya maoni ya mwaka wa 2011 Ladu anasema umoja wa Sudan au kujitenga kwa eneo la kusini kutategemea utekelezaji wa mkataba wa amani wa mwaka wa 2005.

Kwa baadhi itakuwa tofauti kurejea kusini mwa Sudan kwa kuwa wamezowea huduma za kaskazini. Hakuna huduma kusini, pengine zipo lakini chache tu na hakuna huduma nyingi za usafiri. Barabara bado ni chache na ndio zimeanza kujengwa. Wengine watarudi na hata pengine kusaidia juhudi za maendeleo.

Sebit Ernest Apuktong, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Bahr al Ghazal mjini Khartoum, alizaliwa muda mfupi kabla umwagaji damu kati ya eneo la kusini na kaskazini kuanza.

Apuktong anajihusisha na muungano wa vijana wa maendeleo kusini mwa Sudan na huandaa warsha kuwahimiza vijana kutoka kusini na kaskazini waaminiane.

Ingawa Apuktong alikulia katika eneo la kusini wakati alipokuwa mtoto mdogo, anasema angependa siku moja kurejea kuanzisha makundi ya vijana.

Wakaazi wengi wa kusini wanafanya kazi na kuishi kaskazini mwa Sudan. Watoto wao wanaenda shule na kuna usalama. Lakini katika eneo la kusini hakuna usalama wa kutosha na kuna matatizo mengi ya kikabila. Katika sehemu kadhaa watu hubeba bunduki wakati wa mchana. Tatizo pekee la kaskazini ni kwamba mtu hatakiwi kusema lolote dhidi ya serikali.

Susie Taban na Ester David, wasichana wawili wanaofanya kazi katika duka moja la urembo mjini Khartoum wanasema amani kati ya kaskazini na kusini mwa Sudan ni nzuri. Wasudan wote ni wamoja na wanaweza kuyatatua matatizo yao wakiungana. Kwa maoni yao wanataka Sudan iliyoungana na hakuna haja ya Sudan Kusini kujitenga.