1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakaazi wa Rafah wako hatarini kushambuliwa na Israel

11 Aprili 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema tarehe ya kufanyika mashambulizi makubwa ya kijeshi katika mji wa kusini mwa ukanda wa Gaza wa Rafah tayari imepangwa. Lakini hakufafanua wala kutoa tarehe rasmi.

https://p.dw.com/p/4eeFZ
Israel | Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Ohad Zwigenberg/AFP/Getty Images

Katika wiki za hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akisema mara kwa mara kuwa mji wa Rafah unaopakana na Misri ndio ngome ya mwisho ya kundi la Hamas na kwamba mashambulizi eneo hilo hayawezi kuepukika ili kulitokomeza kabisa kundi hilo la wanamgambo ambalo limeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi.

Tamko hilo jipya la Netanyahu limekabiliwa na ukosoaji mkali wa kimataifa hasa kuhusu operesheni zote zilizopangwa za ardhini. Zaidi ya Wapalestina milioni moja ikiwa ni zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza , wamekimbilia katika mji huo, ambao umekuwa ukishambuliwa kwa makombora mara kwa mara. Mji wa Rafah ni sehemu muhimu kunakopita misaada mingi kutoka Misri kwa ajili ya wakazi wa Gaza.

Vikosi vya ardhini vya Israel viliondoka kutoka Khan Younis, mji mwingine wa kusini mwa ukanda huo na kuacha tu kikosi kimoja eneo la kaskazini mwa Gaza ili kudhibiti njia mpya iliyoundwa katikati mwa Gaza na ambayo hutenganisha eneo la kaskazini na kusini.

Cameron awasili Washington kujadiliana Ukraine, Gaza

Wakazi wa Khan Younis, waliohamishwa hadi Rafah, walionekana wakirejea katika mji wao na kushuhudia uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi yaliyodumu kwa miezi sita na kusababisha hadi sasa vifo vya Wapelestina zaidi ya 33,000, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas.

Kabla ya vita, mji huo mdogo ulikuwa na wakazi takriban 250,000 na ulijulikana zaidi kwa kuwa ulikuwa kivuko muhimu katika mpaka na Misri. Kwa sasa hakuna nafasi ya kutosha huko Rafah ambako watu wengi waliohamia katika mji huo wamekuwa wakilazima kuishi katika mazingira duni, kuishi katika mahema, kwenye gari au kulala katika makazi ya muda barabarani.

Operesheni ya kijeshi Rafah: Baadhi waunga mkono na wengine walaani

Vita kati ya Israel na Hamas vimeingia  mwezi wa sita tangu viipoanza Oktoba 7
Wapalestina wakiwa katika eneo lililoshambuliwa kwa kombora la Israel katika nyumba moja mjini RafahPicha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baraza lake la vita wamesisitiza kwamba wataendelea na mpango wa kuivamia Rafah ili kusambaratisha vikosi vinne vya Hamas ambao wanadai wamejificha kwenye mahandaki na kujichanganya miongoni mwa raia waliokimbia makazi yao.

Lakini shambulio hilo lilopangwa limeibua shutuma kali duniani kote, hasa kutoka Marekani, ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel na msambazaji mkubwa wa silaha. Maafisa wa Marekani wameonya kwamba mashambulizi hayo yatakuwa "kosa" ikiwa hakutokuwepo mpango wa kuaminika wa kuhamisha na kuwalinda raia.

Nicaragua yaitaka ICJ iyamuru Ujerumani kutoipatia Israel silaha

Misri pia imeelezea wasiwasi wake kwamba mpango huo unaweza kupelekea jeshi la Israel kuchukua udhibiti wa Ukanda unaofahamika kama Philadelphi, ambao unapatikana kati ya Misri na Gaza, na hivyo raia wanaotafuta usalama kulazimika kukimbilia nchini humo.

Ukosoaji huo hadi sasa haujakuwa na athari kubwa sana kwa Waziri mkuu wa Israel au wakazi wa nchi hiyo. Kura ya maoni ya hivi majuzi iliyoendeshwa na Taasisi huru ya Demokrasia ya Israel yenye makao yake makuu mjini Jerusalem, imeonyesha kuwa takriban robo tatu ya Wayahudi wanaunga mkono upanuzi wa operesheni za kijeshi huko Rafah, huku theluthi mbili ya Waarabu wa Israel wakipinga hatua hiyo.

Wapalestina warejea Khan Younis baada ya Israel kuondoka

Marekani, Misri na Qatar, zimesimamia mazungumzo ya kujaribu kuwezesha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas ambayo yangeliwezesha pia kuachiliwa kwa mateka zaidi wa Israel. Lakini mazungumzo hayo bado yamegonga mwamba na azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo Marekani haikulipinga kwa kura ya turufu, limeongeza shinikizo dhidi ya Israel katika vita vyake huko Gaza.