1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanapiga kura kumchagua rais katika awamu ya tatu

13 Novemba 2017

Wakazi wa  eneo  lililojitenga na taifa la Somalia, Somaliland, leo wanapiga kura ya kumchagua rais wao katika awamu ya tatu. Wamefanya uchaguzi huo wakidhamiria kudhihirisha kuwa na sifa za kidemokrasia 

https://p.dw.com/p/2nVzV
Karte Somaliland Somalia Deutsch
Picha: DW

Pia wanafanya uchaguzi huo wakisisitiza zaidi kupata uhuru wao na kutambulika kimataifa. 

Eneo hilo lililo Kaskazini  mwa nchi hiyo, lenye kabila zenye kujitukuza na imara ukiliganisha na maeneo mengine ya Somalia, lilijitenga mnamo mwaka 1991 na tangu wakati huo linasisitiza kutambuliwa kimataifa.

Wagombea watatu, wanawania nafasi hiyo ya urais, akiwamo mwanasiasa, Muse Bihi, wa chama tawala cha Kulmiye na mpinzani Abdirahman Iro na Faysal Ali Warabe, ambaye aliangushwa katika uchaguzi uliopita  wa 2010.

Mchakato wa upigaji kura ulianza kwa amani asubuhi ya leo, na tuna imani kuwa uchaguzi huu utakuwa wa kipekee  na muhimu kwa nchi nzima,`` amesema Iro wakati akipiga kura.

Uchaguzi katika eneo  hilo hufanywa kila baada ya miaka mitano, hata hivyo, upigaji kura uliahirishwa kwa miaka miwili kutokana na ukame na masuala ya kiufundi. Rais  wa sasa, Ahmed Mohamud Silaanyo, si mgombea katika uchaguzi huu.

Markt in Somalia
Picha: picture alliance/Africa 24 Media/Tim Freccia

Somaliland ina sifa  tofauti na taifa la Somalia

Somaliland ina historia ya kuwa na amani, uchaguzi wenye sifa na mabadiliko makubwa ya kidemokrasia, ambayo yameifanya kuwa tofauti na taifa la  Somalia, na hata nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Katika uchaguzi uliofanyika Somalia mwaka huu, Rais alichaguliwa katika mchakato ambapo viongozi  maalum wa kimila walioteuliwa ndio  walioruhusiwa kupiga kura.

Kabla ya uchaguzi huu wa Somaliland, wagombea wakuu wawili, walishiriki  mjadala uliorushwa katikatelevisheni  na kueleza ajenda zao za kisiasa, wakijikita zaidi katika uchumi, ajira na kutambulika kwa nchi hiyo kimataifa.

 ``Huu ni uchaguzi muhimu sana, kwa vijana, kwani wanahitaji kiongozi ambaye anaweza kuimarisha uchumi na kuleta ajira, ili kila mtu aishi nchini kwake akifurahia maisha,`` amesema mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Ismail Mohammed.

Upigaji  kura unatajwa kuwa muhimu ambapo watu 700,00 walijisajiliwa kwa kutumia mfumo wa elektroniki wa Biometric  .

Hata hivyo, uamuzi wa mamlaka za eneo hilo  kufunga mitandao yote ya kijamii wakati  upigaji kura hadi vituo vitakapofungwa saa 12 jioni kwa saa za Africa Mashariki, ulikosolewa na taasisi ya Human Right Watch wiki iliyopita.

Msemaji wa tume ya uchaguzi, Said Ali Muse alifafanua akisema hatua hiyo ya uzimwaji wa mitandao ya kijamii ni muhimu ili kuzuia muingiliano kutoka katika mipaka ya utawala wa Somalia na udadisi wa matokeo hayo.

Somaliland ambayo ni koloni la zamani la Uingereza, ilipata uhuru wake, mwaka 1960 na baadaye ikajiunga na Somalia . Mwaka 1991, baada ya miaka kadhaa ya vita na serikali kuu mjini  Mogadishu, Somaliland ilijitangazia uhuru wake na kujitenga na  Somalia.

 Mwandishi: Florence Majani(AFPE/AP)

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman