1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya waingia siku ya tatu ya ghasia za waandamanaji na polisi

18 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CtME

NAIROBI:

WaKenya leo Ijumaa wanakabiliwa na siku ya tatu ya maandamano ya upande wa upinzani dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi jana uliomrejesha madarakani rais Mwai Kibaki.Upande wa upinzani unasema kuwa watu wasiopungua wanane wameuawa na polisi kwa kupigwa risasi wakati wa maanadano ya siku mbili ambayo yalipigwa marufuku.Akizungumza na waandishi wa habari jana Alhamisi-kiongozi wa upinzani Raila Odinga ameishutumu serikali ya Kibaki na polisi kwa kuigeuza Kenya kama eneo la mauaji.

Aidha amesema kuwa polisi imewapiga risasi na kuwauwa watu saba katika mitaa ya mabanda Nairobi wakati polisi ikipambana dhidi ya waandamanaji kwa siku mbili mfululizo hiyo jana.Lakini nayo serikali inasema viongozi wa chama cha upinzani cha ODM ndio wanabeba dhamana ya yale yote yanayoendelea.Msemaji wa serikali, Dr Alfred Mutua, ameiambia Deutsche Welle kuwa juhudi zao za kuwashawishi wana ODM kukaa kujadiliana kumaliza mgogoro huo zimeshindikana.

Wafuasi wa upinzani walikaidi marufuku ya serikali ya kutofanya mikutano na wakaingia barabarani kupinga kuchaguliwa tena kwa rais Mwai Kibaki. Polisi ya kuzuia fujo imejihami vilivyo kupambana dhidi ya waandamanaji hao.Mwandishi wa habari wa Deutsche Welle wa mjini Nairobi amesema kuwa mapambano ya jana sanasana yalitokea katika mitaa ya mabanda.Bw Odinga amesema kuwa watu zaidi ya 1,000 wameuawa katika mgogoro ulioanza baada ya uchaguzi wa Disemba 27, ambao upinzani unadai kulikuwa na mizengwe.Kwa mda huohuo bunge la Ulaya limeomba kurejelewa upya kwa uchaguzi.