1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakfu za kisiasa katika wakati mgumu

30 Machi 2012

Wakfu za kisiasa za Kijerumani zilizopo nje ya nchi hiyo zinafanya kazi katika mazingira magumu kama vile wakfu wa Konrad Adenauer uliolazimishwa kufunga ofisi zake nchini Abu Dhabi.

https://p.dw.com/p/14VSr
Wakfu wa Konrad Adenauer
Wakfu wa Konrad AdenauerPicha: KAS-Pakistan

Wakfu wa Konrad Adenauer, wenye makao makuu nchini Ujerumani, umelazimishwa kufunga ofisi zake katika umoja wa falme za Kiarabu. Mwenyekiti wa wakfu huo, Hans-Gert Pöttering, anaiona hatua hii kama ishara ya hatari. Akizungumza na Deutsche Welle (DW), Pöttering alisema "Jambo hili likichukuliwa kama mfano na nchi za Kiarabu, basi itakuwa vigumu sana kuimarisha mazungumzo baina ya watu wenye tamaduni tofauti, jambo ambalo limekuwa likifanywa na wakfu wa Konrad Adenauer." Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ameutaka umoja wa falme za Kiarabu kuubadilisha msimamo wake wa kuzitaka ofisi za wakfu wa Konrad Adenauer zifungwe.

Ofisi za wakfu wa Konrad Adenauer zilizopo Abu Dhabi zilifungwa wiki chache baada ya ofisi za wakfu huo nchini Misri kufungwa pia. Mwaka jana ofisi iliyopo Cairo, pamoja na taasisi nyingine zisiso za kiserikali, zilishutumiwa na serikali ya Misri kupokea fedha kwa namna isiyo halai na pia kufanya kazi bila ya kuwa na vibali vyote vinavyotakiwa. Uamuzi wa serikali ya Misri umeziathiri pia wakfu nyingine kutoka Ujerumani kama vile wakfu za Friedrich Ebert, Friedrich Naumann na Hanns Siedel ambazo pia zina ofisi nchini humo.

Hans-Gert Pöttering kutoka wakfu wa Konrad Adenauer
Hans-Gert Pöttering kutoka wakfu wa Konrad AdenauerPicha: picture-alliance / dpa

Nazo wakfu za Heinrich Böll na Rosa Luxemburg, ambazo zilikuwa na mpango wa kufungua ofisi mjini Cairo, zimeeleza kwamba hatua hii inaurudisha nyuma mpango huo. Uongozi wa wakfu hizo umeeleza kwamba kinachosuburiwa sasa ni uchaguzi kufanyika Misri mwezi Mei mwaka huu na kwamba lipo tumaini kuwa hali itaboreka baada ya uchaguzi kufanyika. Mkuu wa kitengo cha masuala ya Asia na nchi za Pacific kutoka wakfu wa Friedrich Ebert, Jürgen Stetten, amesema kuwa jambo lililotokea Misri lina athari kwa nchi nyingine katika eneo hilo.

Maandalizi bora kwa ajili ya kazi za nje ya nchi

"Ni kama vile mahali palipo na mifumo miwili tofauti ya umeme. Unahitaji kuwa na 'adapter' kwa ajili ya kila mfumo. Kazi nchini Pakistan inahitaji 'adapter' maalum ya Kipakistan," anasema Babak Khalatbari, mkuu wa ofisi ya wakfu wa Konrad Adenauer mjini Islamabad, Pakistan. Anaeleza kwamba kazi wanayoifanya nchini humo inaweza kuonekana rahisi lakini ukweli ni kwamba inahitaji mtu awe na ufahamu mkubwa juu ya nchi anayofanya kazi, ufahamu juu ya mila na desturi na pia ufahamu wa lugha.

Jürgen Stetten kutoka wakfu wa Friedrich Ebert
Jürgen Stetten kutoka wakfu wa Friedrich EbertPicha: Friedrich Ebert Stiftung

Wawakilishi wapatao 300 kutoka wakfu mbali mbali za Ujerumani wanafanya kazi katika dunia nzima. Kwa kawaida wakfu hizo, ambazo mara nyingi huwa na mtazamo wa kisiasa unaoendana na chama cha siasa kilichounda wakfu huo, hukaa pamoja na wenyeji wao na kisha kubuni miradi ya pamoja ya maendeleo.

Maandalizi ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi yanachukuliwa kama jambo la muhimu sana. Watu wanaotazamiwa kuwa wakuu wa ofisi kwa kawaida huandaliwa katika kipindi cha miezi sita. Mbali na kufundishwa namna ya kusimamia miradi, wanapata pia mafunzo ya lugha, utamaduni na taarifa za muhimu kuhusu nchi watayokwenda kufanya kazi. Tim Petschulat, ambaye ni kiongozi wa ofisi ya wakfu wa Friedrich Ebert nchini Yemen, anaona kwamba maandalizi haya ni ya muhimu sana. "Hata kama watu wakielewana vizuri, hawawezi kufanikisha mradi ikiwa hawaelewani katika upande wa kiutamaduni." Naye Gerhard Wahlers, ambaye ni makamu katibu mkuu wa wakfu wa Konrad Adenauer, anakubali pia kwamba maandalizi ni jambo la msingi. "Ni lazima mtu atambue kwamba akiwa nje ya Ujerumani, hata kama ikiwa Marekani au Ulaya, yupo mahali ambapo pana utamaduni wa tofauti."

Mazingira magumu ya kufanyia kazi

Wakfu za kisiasa hupewa masharti tofauti tofauti katika nchi zinamofanya kazi. Lakini jambo ambalo ni sawa sawa kwa kila mfanyakazi wa wakfu wa kisiasa ni kwamba ofisi yake iko mbali na makao makuu ambayo yako Ujerumani. Hivyo wafanyakazi wa wakfu hizo hubeba dhamana kubwa na kupewa majukumu mengi. Kujitoa kwa wafanyakazi pamoja na ubunifu ndio mambo yanayozipa wakfu uhai. Kwa kawaida wakfu hizo hushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali au na mabunge. Wakati mwingine nchi husika hazipendezwi na jambo hilo na kuona kwamba wakfu zinataka kuingilia mambo ya serikali. Khalabatri, anayefanya kazi katika wakfu wa Konrad Adenauer nchini Pakistan anasema: "Hebu fikiria ingekuwaje kama wakfu kutoka nje zingekuja hapa Ujerumani na kuanza kulishauri bunge. Hata sisi tungejiuliza imekuwaje hadi wakapewa nafasi ya kufanya hivyo?"

Babak Khalatbari wa wakfu wa Konrad Adenauer Pakistan
Babak Khalatbari wa wakfu wa Konrad Adenauer PakistanPicha: Matthias Koch

Inahitaji umakini mkubwa wa kufahamu namna ya kufanya kazi na taasisi katika nchi za kigeni. Kwa mfano, nchini Zimbabwe, wafanyakazi wa wakfu za kisiasa huchunguzwa kila wakati na wako katika hatari ya kufukuzwa kutoka katika nchi hiyo wakati wowote. Hata nchini China na Vietnam, serikali huchunguza kwa makini kabisa kujua mambo yanayofanywa na wakfu za kisiasa. Katika nchi nyingine si hali ya kisiasa bali hali ya usalama inayozifanya kazi za wakfu kuwa ngumu. Mfano mmojawapo ni nchi ya Yemen ambapo matendo ya kigaidi na utekaji nyara unahatarisha maisha ya wafanyakazi.

Mwandishi: Sabine Hartert-Mojdehi

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman