1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Iraq wakosa ajira nchini Syria

Scholastica Mazula24 Machi 2008

Zaidi ya raia milioni wa Iraq wanaishi Nchini Syria bila kazi.Hali hii inasababishwa na wao kutokuwa na kitu cha kufanya kitendo kinachowafanya waitwe watu wasiokuwa na ajira.

https://p.dw.com/p/DTbm
Ndege za kivita za Majeshi ya Marekani zikiwa katika anga la Iraq kuendelea na kile wanachokiita ukombozi wa Iraq June 19, 2001.Picha: AP

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa- UNHCR; limesema kuna zaidi ya wakimbizi milioni moja nukta tano raia wa Iraq nchini Syria na kwamba wakijaribu kutafuta kazi wanaweza kupoteza haki zao za ukimbizi.

Kwa mujibu wa UNHCR, wakimbizi wote ambao walikuwa na ujuzi mbalimbali kama udaktari, wahandisi, wasanii, wafanyabiashara na wanariadha wamekuwa hawana cha kufanya na badala yake kukaa bila kazi nchini Syria.

Daktari Jassim Alwan ambaye alikimbi kutoka mjini Baghdad baadaa ya kukamatwa na majeshi ya Marekani mwaka 2003, anasema wamekuwa wakiitwa watu wasiyokuwa na ajira.

Dokta Alwan anasema kitu kingine kilichomfanya akimbie nikule kudharirishwa kama wanyama kitendo kinachofanywa na majeshi ya marekani yaliyodai kuwa wakombozi wa Iraq.

Anasema hivi sasa hana kazi na kitu anachokifanya ni kukaa tu na usiku unapoingia hawezi kulala kwa sababu inambidi kufikilia sana juu ya maisha ya baadaye ya familia yake kitu ambacho kinawakabili Wairaq wengi nchini humo.

Wakimbizi wengi kutoka Iraq wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kukusanyika katika migahawa ya chai wakinywa chai ya Kiiraq na wengine kuvuta sigara.

Hata hivyo Salim Khattab ambaye awali alikuwa mhandisi kutoka Mosul ameliambia Shirika la habari la IPS kwamba siyo kila mtu anaweza kununua sigara.

Anasema wengi wao hawana fedha baada ya kukaa bila kazi kwa kipindi kirefu na hivyo kutopokea mshahara wa aina yoyote.

Anasema kwa ujumla hali ya wakimbizi kutoka Iraq nchini Syria siyo nzuri kutokana na wao kutopewa nafasi ya kufanya kazi na kujiingizia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Wiki iliyopita Shirika la Kimataifa linaloshughulika na masuala ya wahamiaji-IOM, lilisema kiasi cha Wairaq milioni mbili nukta saba wamepoteza makazi yao nchini Iraq na wengine milioni mbili nukta nne wamekimbilia nchi za kigeni hasa Jordan na Syria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya IOM hali ya maisha ya Wairaki waliopoteza makazi yao na ya wakimbizi inazidi kuwa mbaya.

Msemaji wa IOM, Jemini Pandya ameliambia shirika la habari la IPS kwamba kuna kiwango kidogo sana cha haki za kibinadamu ambacho wanakipata Wairaq.

Taarifa hiyo ya IOM imesema zaidi ya asilimia sabini na tano ya Wairaq hawapati msaada wa chakula unaotolewa na Serikali na asilimia ishirini hawapati maji safi na salama,na pia asilimia thelathini na tatu hawapati huduma ya madawa wanayohitaji.

Hata hivyo ni asilimia ishirini tu ya Wairaq wanaopata misaada ya kibinadamu kutoka kwa mashirika mbalimbali ya misaada.