1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Mali wako mashakani

12 Aprili 2013

Wakimbizi 74 elfu wa Mali wamekwama katika jangwa la Mauritania wakikumbwa na ukosefu wa maji na idadi ya vifo vya watoto ikizidi kuongezeka,linasema shirika la madaktari wasiokuwa na Mipaka-Medecins Sans Frontiere.

https://p.dw.com/p/18EoA
Wakimbizi wa Mali karibu na mpaka na MauritaniaPicha: DW/J.M. Oumar

Mzozo wa Mali umepelekea zaidi ya watu laki mbili na 70 elfu kuyapa kisogo maskani yao na kuranda randa ndani nchini huku wengine zaidi ya laki moja na 70 elfu wakikimbilia katika nchi jirani na hasa Burkinafasso,Mauritania na Niger.

Katika jangwa la Mauritania ambako hali ya hewa inapindukia nyuzi joto 50 kivulini, kambi ya wakimbizi ya Mbera inawapokea watu 74 elfu "walionasa jangwani" - kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Madaktari Wasiokua na Mipaka-Medecins Sans Frontièren-MSF.Watu hao wamekimbia mapigano,chuki za kikabila,ukosefu wa chakula na kuvurugika mfumo wa huduma za jamii.

Ripoti hiyo inazungumzia kuhusu "hali mbaya kupita kiasi" inayowakumba watu hao wanaotegemea moja kwa moja msaada kutoka nje kuweza kunusurika. "Chakula kipo cha kutosha,lakini hakuna maji"- amesema Marie-Christine Ferir anaesimamia operesheni za dharura katika shirika hilo la madaktari wasiuwa na mipaka.

Watoto walioanza kuingia katika kambi hiyo tangu januari mwaka huu,hali yao ya afya imeharibika na wanaonyesha dalili za ukosefu wa lishe bora-amesema bibi Marie-Christine Ferir na kuongeza watoto kati ya 23 na 24 wanakufa kila siku katika kambi ya Mbéra.

Mazungumzo ya kuleta suluhu yaharakishwe

Tuareg in Burkina Faso
Watuareg wamekimbilia Burkina FasoPicha: DW/K. Gänsler

Katika ripoti yake shirika la Medecins Sans Frontiere-MSF inasisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kutolewa misaada kwa wakati wote unaohitajika.

"Mivutano ya kikabila na kisiasa ndiyo chanzo cha hali hii na hakuna dalili kama wakimbizi watarejea nyumbani haraka" shirika la MSF limesema.

Ili kumaliza mzozo,shirika la kimataifa linalosimamia mizozo limeihimiza serikali ya mjini Bamako ianzishe haraka juhudi za kuzipatanisha jamii nchini Mali.Miongoni mwa mengineyo shirika hilo linaisihi serikali ianze mazungumzo na jamii ya watuareg na waarabu.

Uchaguzi utaitishwa Julai

Wakati huo huo waziri mkuu Diango Sissoko wa Mali akiwa ziarani Gao amesema uchaguzi utaitishwa kama ilivyopangwa mwezi Julai mwaka huu licha ya shaka shaka kama serikali itaweza kweli kudhibiti hali ya mambo katika maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo.

Hiyo ilikuwa ziara ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa serikali tangu vikosi vya Ufaransa vilipoanzisha opereshini ya kuwaandama wanamgambo wa itikadi kali Januari mwaka huu.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef