1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Sudan wateseka Sudan Kusini

4 Aprili 2024

Wakimbizi wa Sudan walioko mjini Juba nchini Sudan Kusini wanapitia madhila makubwa, wakiwa na simulizi za kuhuzunisha kufuatia kukosa huduma kadhaa za msingi kama vile chakula, maji na vyoo.

https://p.dw.com/p/4eR3h
Sudan Kusini na Suda
Hali mbaya ya wakimbizi wa Sudan walioko Sudan Kusini imekuwa ikizidi kila uchao.Picha: LUIS TATO/AFP

Vita vinavyoendelea kati ya Mkuu wa Majeshi ya Sudan, Jenerali Al Fattah Burhan, na makamu wake wa zamani na kiongozi wa Kikosi cha Wanamgambo wa RSF, Mohamed Hamdan Daglo, vinazidi kuchukua mkondo mpya.  

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linasema zaidi ya watu 1,500 wanaokimbia makaazi yao kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan wanawasili Sudan Kusini kila siku.

Kambi moja ya wakimbizi iliyopo katika Kaunti ya Renk imekuwa ikiwapokea watu kutoka Sudan karibu mwaka mzima sasa.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waomba Wasudan wasisahauliwe

"Hatujui vita vitakwisha lini, ndiyo maana tupo hapa. Hatujui ni lini. Ni ngumu sana na ni vita vigumu sana. 
Hakuna vituo vya afya, hakuna maji. Hatujaona hali kama hii katika nchi yetu ya Sudan." Alisema mmoja wa wakimbizi hao.

Mwengine alilalamika kwamba hali zao si nzuri kwa kuwa hawana maji ya kutosha. "Watu wanateseka kwa sababu ya maji. Hakuna chakula cha kutosha kwa ajili yetu. Watoto wadogo wanatapika na hakuna choo wala shule." 

Wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

Mkimbizi mwengie alisema wanachoomba wao ni amani tu. "Amani ya kweli. Sisi ndio tunateseka na watoto wetu wadogo. Kwa sasa Wasudani wanateseka tu bila chakula, bila maji bila dawa."

UNCHR yazinduwa mpango wa wakimbizi


Shirika la UNCHR kupitia ofisi zake za Nairobi, Kenya, imezindua mpango wa kukabiliana na wakimbizi wa mwaka 2024 ili kupunguza mzigo wa wakimbizi walioko nchini Sudan Kusini, Ethiopia, Kenya na Uganda.

Katika mpango huo shirika hilo linatafuta dola za Marekani bilioni 1.4 kusaidia wakimbizi milioni 2.33 katika nchi hizo nne.

Mkurugenzi wa shirika hilo kwa Afrika Mashariki, Pembe ya Afrika na maeneo ya Maziwa Makuu, Mamadou Dian Balde, anasema huo ni mpango wa kuokoa maisha.

Wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

Soma zaidi: Watoto 13 wafa kila siku kwa utapiamlo Darfur - MSF

"Yote ni kuhusu huduma za kimsingi na pia kubadilisha kadiri inavyowezekana maisha ya jamii. Hoja tunayoelezea hapa ni juu ya kuomba rasilimali endelevu na kutumia jamii tulizonazo, na kwa sasa tunaendana na mabadilko yaliyopo." Anasema mkurugenzi huyo.

Wakimbizi wa Sudan Kusini nao wako taabani

Hali ngumu pia wanayo wakimbizi wa Sudan Kusini walioko mataifa jirani.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Uganda, Mathew Grentsil, anasema kuna uandikishwaji duni shuleni kwa watoto wa Sudan Kusini katika kambi za wakimbizi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan nchini Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

"Tuna takribani, watoto 480,000 wa Sudan Kusini walioandikishwa shuleni, ukiacha idadi ya watoto wengine 206,000 waliokosa shule, Hiyo ina maana gani? Ukiangalia kwa umakini, utagunduwa kuwa wengi wa wale ambao hawako shuleni ni wale walio katika kiwango cha shule ya sekondari. Kwa hivyo, kwa hali hii mambo sio mazuri hapa Sudan Kusini, Tunalo kundi kubwa, vijana wa kiume na wa kike, ambao hawajaenda shule. Swali ni je huko mbeleni itakuwaje?" Anauliza Grentsil.

Soma zaidi: Burhan amfuta kazi Dagalo kama Naibu wa Baraza Tawala Sudan

UNHCR inasema kuwa nchi ya Uganda ndio yenye wakimbizi wengi zaidi barani Afrika, kwani inatoa hifadhi kwa zaidi ya watu milioni 1.5.

Asilimia 57 ya wakimbizi hao wanatoka Sudan Kusini, asilimia 32 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo, asilimia tatu kutoka Somalia na asilimia nyingine tatu wanatoka Burundi.