1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima Ujerumani waandamana kupinga kuondolewa ruzuku

8 Januari 2024

Wakulima Ujerumani wameanza maandamano ya wiki nzima kupinga mipango ya kuondolewa kwa ruzuku za kilimo, uamuzi ambao ni sehemu ya juhudi za serikali za kurekebisha mikakati yake ya matumizi katika miaka inayokuja.

https://p.dw.com/p/4ayIC
Maandamano ya wakulima mjini Berlin
Maelfu ya wakulima wa Ujerumani wamefanya maandamano makubwa kupinga hatua za serikali za kubana matumizi.Picha: Michael Kuenne/PRESSCOV/ZUMA Press Wire/picture alliance

Misafara ya matrekta na malori imeonekana barabarani tangu majira ya asubuhi na polisi imesema kwenye baadhi ya maeneo wakulima wamezifunga njia muhimu na kutatiza kabisa shughuli za uchukuzi.

Maandamano hayo yanafanyika licha ya serikali ya mseto ya Kansela Olaf Scholz kuachana na mipango ya kutaka kuifuta mara moja ruzuku ya mafuta yanayotumika kwenye kilimo na badala yake kuiondoa kwa awamu kuanzia mwaka ujao hadi 2026.

Soma pia: Serikali ya Ujerumani yakabiliwa na mwaka mgumu mbele yake 

Serikali pia imeachana na mipango ya kuifuta nafuu ya kodi inayotolewa kwenye vyombo vya moto vinavyotumika kwenye sekta ya kilimo na misitu.

Hata hivyo vyama vya wakulima vimesema mabadiliko yote hayo bado hayatoshi.