1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi wa Irak wapiga kura kumchagua rais mpya na bunge

Josephat Nyiro Charo23 Julai 2009

Umoja wa Mataifa waonya dhidi ya kura ya maoni kuhusu eneo la Kirkuk

https://p.dw.com/p/Iw3q
Kiongozi wa Wakurdi kaskazini mwa Irak Massoud BarzaniPicha: AP

Eneo la Wakurdi linalojitawala kaskazini mwa Irak linajiandaa kufanya uchaguzi kumchagua rais na bunge jipya. Uchaguzi huo unafanyika huku kukiwa na mzozo wa ardhi na serikali kuu ya Irak mjini Baghdad na wasiwasi ukizidi kuhusu mauzo ya mafuto katika nchi za kigeni unaoweza kuzusha vita. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umewaonya Wakurdi wa Irak wasifanye kura ya maoni kuamua ikiwa eneo la Kirkuk lenye utajiri mkubwa wa mafuta linapaswa kuwa sehemu ya Kurdistan.

Rais Massud Barzani wa Kurdistan, anatarajiwa kushinda kwa kishindo uchaguzi wa siku ya Jumamosi na kuendelea kubakia madarakani huku chama chake cha Kurdistan Democratic Party, KDP, na chama cha Patriotic Union of Kurdistan cha rais wa Irak, Jalal Talabani, vikitarajiwa kuzoa viti vingi katika bunge la eneo hilo. Wapiga kura zaidi ya milioni 2.5 wana haki ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Vyama hivyo viwili ambavyo vimedhibiti siasa za eneo la Kurdistan kwa miongo kadhaa, vimewasilisha orodha ya pamoja ya majina ya wagombea wapya katika juhudi ya kutoa taswira ya kufanya mageuzi. Hata hivyo vinakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wagombea wanaotaka kuvunja udhibiti wa kisiasa katika ngome zao.

Zaidi ya wanajeshi 100,000 wa kikurdi katika jeshi la Irak wameanza kupiga kura tangia jana, pamoja na maafisa wa polisi, wafungwa na wagonjwa, kabla siku yenyewe ya uchaguzi Jumamosi ijayo. "Ninafurahi kuweza kutumia haki yangu ya kidemokrasia," amesema Hadi Sultan, mwanajeshi wenye umri wa miaka 33, wakati alipokuwa akipiga kura katika kituo cha kupigia kura mjini Baghdad.

Uchaguzi wa siku ya Jumamosi ijayo unafanyika miezi sita baada ya maeneo mengine ya Irak kufanya uchaguzi wa mikoa na huku Marekani ikijiandaa kuwaondoa wanajeshi wake wote kutoka nchini humo ifikapo mwaka 2011.

Hali ya wasiwasi

Kipindi cha kuelekea uchaguzi wa Jumamosi hali ya wasiwasi kati ya rais wa eneo la Kurdistan, Massud Barzani, na serikali kuu ya Irak mjini Baghdad, inayoongozwa na waziri mkuu Nuri al Maliki, imekuwa ikiongezeka kutokana na maeneo 16 yanayozozaniwa ikiwa ni pamoja na eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Kirkuk na sehemu za majimbo matatu ambayo kitamaduni yamekuwa yakikaliwa na Wakurdi; Diyala, Nineveh na Salaheddin.

Wakati wa uvamizi wa Marekani mnamo mwaka 2003, waasi wa kikurdi waliokuwa wameupiga vita utawala wa kiongozi wa Irak aliyong´olewa madarakani, marehemu Saddam Hussein, waliyakalia maeneo mengi miongoni mwa yale yanayozozaniwa. Waasi hao wa zamani sasa wanashika doria pamoja na wanajeshi wa jeshi la Irak, hivyo kusababisha kitisho cha kuzuka vita.

Jalal Talabani
Rais wa Irak Jalal TalabaniPicha: AP

Rais wa eneo la Kurdistan, Massoud Barzani, amesema Jumapili iliyopita kwamba hatokubali madai ya muda mrefu kuhusu eneo la Kirkuk. Badala yake kiongozi huyo amesisitiza swala hilo litatuliwe kupitia kura ya maoni kwa mujibu wa katiba ya Irak, na kuzisaidia familia zilizoyakimbia makaazi yao kurejea makwao, licha ya upinzani mkali kutoka kwa jamii za Waarabu na Waturkimenia, watu wenye asili ya kituruki.

Waziri wa utamaduni na sanaa wa eneo la Kurdistan, Sammy Shourash, amesema serikali mpya ya Kurdistan itakayoundwa itakabiliwa na changamoto kubwa, nzito ikiwa usuluhisi wa mzozo wa mipaka na wa kikatiba na serikali kuu mjini Baghdad. Dyandar Zebari, mratibu wa mahusiano kati ya serikali ya Kurdistan na Umoja wa Mataifa, ameongeza kusema kuwa serikali hiyo pia itatakiwa kufikia makubaliano na serikali ya Baghdad juu ya kugawana raslimali za nishati kutoka visima vya mafuta vilivyo kaskazini mwa Irak.

Kura ya maoni

Umoja wa Mataifa umewatolea wito Wakurdi wa Irak wasishinikize kufanya kura ya maoni kuhusu eneo la Kirkuk, ukisema hatua hiyo huenda ikachochea mzozo usio mithili. Umoja huo unaamini kura hiyo ya maoni itakuwa hatari na huenda izushe mapigano kati ya makundi yanayohasimiana huku Irak ikikaribia kuwa thabiti.

Mwanadiplomasia wa nchi za magharibi anayeshiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo, amesema Umoja wa Mataifa hautaunga mkono kura ya maoni yenye machafuko. Mvutano huo baina ya Wakurdi na Warabu juu ya ardhi na mafuta unaonekana kuwa kitisho kikubwa kwa usalama wa Irak.

Mwandishi: Josepaht Charo/RTRE

Mhariri: Othman Miraji