1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi waendelea na mapambano dhidi ya IS -Kobane

Admin.WagnerD21 Oktoba 2014

Wapiganaji wa kikurdi katika mji wa Kobane nchini Syria wanaendelea kupambana vikali na wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS huku wakisubiri kupigwa jeki na wenzao kutoka Iraq

https://p.dw.com/p/1DZ8k
Picha: Getty Images

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Syria Rami Abdel Rahman amesema wanamgambo wa IS walifanya mashambulizi kutoka kila upande wa mji wa Kobane jana jioni huku mapigano makali yakiripotiwa kuendelea katika mji huo wa mpakani kati ya Syria na Uturuki

Wanamgambo hao wamewaleta wapiganaji zaidi kutoka Jarabulus hadi magharibi mwa Kobane huku mashambulizi makali yakirejewa katikati mwa mji huo kufikia mwishoni mwa jana.

IS wazidisha mashambulizi Iraq

Waasi hao wa IS pia wanaonekana kuzidisha makali ya mashambulizi yao nchini Iraq hasa katika mji unaodhibitiwa na wakurdi wa Qara Tapah ambapo kiasi ya watu kumi wameuawa na kusababisha maelfu ya wakaazi wa mji huo kutoroka.

Watu wakitizama mashambulizi ya Marekani dhidi ya IS mjini Kobane
Watu wakitizama mashambulizi ya Marekani dhidi ya IS mjini KobanePicha: picture alliance/abaca/Murat Kula

Mashambulizi hayo ya IS yanafanyika huku juhudi za jumuiya ya kimataifa kukabiliana na kitisho hicho cha IS zikiongezeka. Mbali na Marekani kuwadondoshea wapiganaji wa kikurdi silaha mjini Kobane hapo jana, Uturuki imesema itawasaidia wapiganaji wa kikurdi wa Iraq.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema nchi yake itasaidia katika kuwasaidia wapiganaji wa kundi la Peshmerga la Iraq kuingia Syria kuelekea Kobane kuwasaidia wenzao kukabiliana na wanamgambo wa IS.

Hata hivyo bado Uturuki imekataa kuwapa silaha na kuwaruhusu wapiganaji wa kikurdi wa Uturuki kuvuka mpaka na kuingia Syria au Iraq kupigana.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya,Umoja huo umeihimiza Uturuki kufungua mipaka yake kwa ajili ya kupelekwa kwa misaada mbali mbali kwa watu wa Kobane.

Marekani na Uturuki zawasaidia wakurdi

Akizungumzia kudondoshwa kwa silaha za aina mbali mbali Kobane kwa ajili ya kuwahami wapiganaji wa kikurdi,waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ni vigumu mno kulipa kundi lolote linalopigana dhidi ya IS mgongo.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut CavusogluPicha: picture alliance/AA/M. Ali Ozcan

Marekani na washirika wake wamefanya mashambulizi 135 ya angani dhdi ya IS karibu na mji wa Kobane lakini ilikuwa haijawahi kutoa silaha moja kwa moja kwa wakurdi wanaokabiliana na IS.

Licha ya hayo, Marekani imesisitiza kuwa mkakati wake wa kukabiliana na kundi hilo la dola la kiislamu bado linatuama zaidi nchini Iraq ambako IS wanayadhibiti maeneo makubwa ya wasunni kaskazini na magharibi mwa Baghdad tangu mwezi Juni mwaka huu.

Waziri mkuu wa Iraq Haidar al Abadi yuko mjini Tehran nchini Iran hii leo kwa mazungumzo na viongozi wa Iran kuhusu vita dhidi ya IS. Waasi hao wakijihadi wanadihibiti miji kadhaa iliyoko kilomita chache karibu na mpaka na Iran na Tehran inaunga mkono vita dhidi yao.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri:Josephat Charo