1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Wakuu wa kijeshi wa China na Urusi wakutana Beijing

Sylvia Mwehozi
30 Oktoba 2023

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu ameinyoshea kidole Marekani kwamba inachochea mivutano ya kikanda ili kudumisha mamlaka yake katika siasa za kikanda na kuonya hatari ya mataifa makubwa kukabiliana.

https://p.dw.com/p/4YBpf
China Peking | Vorbereitungen | Xiangshan Forum
Picha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Akizungumza katika jukwaa la kijeshi la China la Xiangshan ambalo ni tukio kubwa la kila mwaka la diplomasia ya kijeshi, Shoigu ameishutumu Marekani na washirika wake wa kanda ya Asia na eneo la bahari ya Pasifiki kwamba wanadhoofisha utulivu katika eneo hilo, akiongeza kuwa Marekani inahujumu kwa makusudi mkakati wa msingi wa utulivu na usalama wa kimataifa kwa kutaka kudumisha utawala wake wa siasa za kikanda na kimkakati.

Soma pia: Putin: Urusi na China haziundi muungano wa kijeshi

Aidha waziri huyo wa ulinzi wa Urusi ameishutumu Marekani na washirika wake wa nchi za Magharibi kwamba wanatoa kitisho dhidi ya Urusi kupitia "upanuzi wa mashariki wa jumuiya ya kujihami NATO", na kuonya hatari ya mzozo wa moja kwa moja baina ya mataifa yaliyo na nguvu ya nyuklia na kusababisha athari kubwa.

Sergei Shoigu
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei ShoiguPicha: via REUTERS

"Baada ya kuibua mzozo mkubwa barani Ulaya, nchi za Magharibi zinataka kupanua uwezekano wa migogoro katika eneo la Asia-Pasifiki na pande nyingine. Ushiriki wa moja kwa moja wa nchi zinazomiliki silaha za nyuklia katika mapambano kunazidisha hatari za kimkakati. Hivi majuzi, kumekuwa na majaribio ya kupeleka uwezo wa nguvu wa NATO katika eneo la Asia-Pasifiki."

Soma kuhusu:  Waziri wa mambo ya nje wa China aanza ziara yake Marekani

Akigusia mzozo wa Ukraine, waziri huyo amebainisha kwamba Moscow iko tayari kwa mazungumzo "ikiwa masharti yatakuwa sawa".

Jukwaa hilo la kijeshi la China la siku tatu lilifunguliwa na afisa wa ngazi ya pili wa kijeshi wa China Zhang Youxia bila ya uwepo wa jenerali Li Shangfu ambaye alifutwa kazi wiki iliyopita kama waziri wa ulinzi wa China. Zhang amesema Beijing "iko tayari kuendeleza ushirikiano wa kijeshi na Washington kwa misingi ya kuheshimiana na ushirikiano wenye maslahi sawa."

Bila kuitaja moja kwa moja Marekani, afisa huyo wa China alizikosoa nchi fulani ambazo amesema "zinaendelea kuchochea matatizo duniani."

Zhang Youxia na Vladimir Putin
Afisa wa ngazi ya pili wa kijeshi wa China Zhang Youxia akisalimiana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mwaka 2017Picha: picture-alliance/S.Karpukhin

"Wanazusha misukosuko ya kimakusudi, kuingilia masuala ya kikanda, kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuchochea mapinduzi. Wanakoweka mikono yao hakuna utulivu. Wakati wa kushughulikia migogoro ya kikanda, mara zote wanaunga mkono upande mmoja kwa njia isiyo ya haki, na hivyo kufanya hali kuwa ngumu zaidi kushughulikia. Wanaongeza mafuta kwenye migogoro kwa kutoa silaha na kuanzisha vita vya kiwakala. Wanafaidika kwa gharama ya wengine.

Ushirikiano wa China na Urusi kijeshi: Urusi na China zafanya luteka za pamoja za kijeshi

Zhang ametoa suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Ukraine na usitishwaji wa mara moja wa mapigano na kukomeshwa ghasia katika pande zote za mzozo wa Isreal na Palestina na kuanza mapema mazungumzo ya amani.

Wawakilishi wa kijeshi kutoka nchi kadhaa ikiwemo Marekani na Urusi wanahudhuria tukio hilo, ambalo linatumiwa na China kusisitiza ushirikiano wake wa kijeshi na mataifa mengine na mkakati wa uongozi wa kikanda.