1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa nchi mbalimbali wampongeza Macron

John Juma
8 Mei 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametaja ushindi wa Macron kuwa ushindi wa Ulaya na wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa. Rais Putin wa Urusi amemhimiza Macron kusuluhisha mgawanyiko kati ya Urusi na Ufaransa

https://p.dw.com/p/2camy
Frankreich Emmanuel Macron hält Rede nach Wahl
Picha: REUTERS/Pool/L. Bonaventure

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wamempongeza Emmanuel Macron kwa ushindi wake wa jana kwenye uchaguzi wa duru ya pili ya urais nchini Ufaransa, huku kukiwa na hisia mchanganyiko juu ya ushindi wa mwanasiasa huyo kijana anayefuata siasa za mrengo wa kati akiunga mkono Umoja wa Ulaya.

Ushindi kwa Umoja wa Ulaya

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani  kupitia msemaji wake naye amempongeza Macron akisema ushindi wake ni ushindi wa Ulaya iliyo thabiti na iliyoungana na pia ushindi wa urafiki kati ya Ujerumani na Ufaransa.

"Ninayo furaha tele kuwa Wafaransa wamechagua mafanikio ya mustakabali wa Umoja wa Ulaya," ni kauli yake Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, huku Rais wa Baraza la Umoja huo, Donald Tusk, akisema Wafaransa wamechagua uhuru, usawa na utangamano na wamesema "la kwa habari bandia".

Wafuasi wa Macron washangilia ushindi
Wafuasi wa Macron washangilia ushindiPicha: picture alliance/dpa/abaca/E. Blondet

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, amesema kuwa ushindi wa Macron ni ishara ya ushindi dhidi ya wabinafsi na mbinu zao katika Umoja wa Ulaya na inaashiria imani kwa Umoja wa Ulaya. Afisa mkuu katika baraza lake la mawaziri, Yoshihide Suga, amesema anatarajia mshikamano.

"Tunatumai kuendelea kuimarisha mahusiano ya nchi hizi mbili chini ya utawala mpya na kuzidisha ushirikiano katika masuala mbalimbali yanaikabili jamii ya kimataifa."

Wakuu wa nchi wahimiza ushirikiano na Macron

"Hongera kwa Emmanuel Macron kwa ushindi wako mkubwa kuwa rais mpya wa Ufaransa. Ninatarajia kushirikiana nawe." Ni kauli ya rais wa Marekani Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter akimpongeza Macron.

Rais Vladimir Putin wa Urusi amemhimiza Macron kusuluhisha mgawanyiko mkubwa uliopo kati ya Urusi na Ufaransa na washirikiane katika kupambana na kitisho cha ugaidi. "Raia wa Ufaransa wamekutwika jukumu la kuongoza nchi katika wakati mgumu kwa Ulaya na kwa dunia kwa jumla. Kuongezeka kwa kitisho cha ugaidi, mapigano ya itikadi kali, kuongezeka kwa mizozo na kuyumba kwa eneo zima. Katika hali hizi, ni muhimu kuishinda hali ya kutoaminiana na tushirikiane ili kuhakikisha uthabiti wa kimataifa na usalama," alisema Putin.

Aliyekuwa mshindani wa Macron Marine Le Pen
Aliyekuwa mshindani wa Macron Marine Le PenPicha: Reuters/C. Platiau

Kutoka Uingereza, Waziri Mkuu Theressa May alimpongeza Macron huku akisema Ufaransa ni miongoni mwa marafiki wa Uingereza na anatumai kushirikiana na rais huyo mpya kuhusu mambo kadhaa wa kadha. Pia walijadiliana kuhusu Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Viongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia zampongeza Le Pen

Hata hivyo, nchini Uholanzi, kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia, Geert Wilders, amempongeza Marine Le Pen aliyeshindwa na Macron kwenye uchaguzi huo wa jana, akisema mamilioni ya watu walimpigia kura. Kauli sawa na hiyo imetolewa na mkuu wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia nchini Austria, Heinz-Christian Strache, akisema Le Pen anastahili heshima, kwani kuanzia sasa amepata nguvu zaidi kuwa mpinzani dhidi ya Macron.

Mwandishi: John Juma/AFPE/

Mhariri: Mohammed Khelef