1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walemavu wa ngozi Malawi hatarini

John Juma7 Juni 2016

Visa vya walemavu wa ngozi kuuawa Malawi vimeongezeka katika miaka miwili iliyopita. Watu 4 akiwemo mtoto waliuawa Aprili mwaka huu. Jumla ya watu 18 wameuawa tangu Novemba 2014. Polisi wamelaumiwa kwa kutowajibika.

https://p.dw.com/p/1J1oh
Walemavu wa ngozi nchini DRC.
Walemavu wa ngozi nchini DRC.Picha: DW/S. Mwanamilongo

Kuongezeka kwa visa vya kuuawa kwa watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi nchini Malawi kumeonyesha udhaifu wa mikakati ya kukabili janga hilo, ambalo limesababisha watu hao kuishi kwa uwoga. Kulingana na ripoti ya shirika la kutetea haki za bindamu Amnesty International, tangu Novemba mwaka 2014, watu 18 wameuawa, watano kutekwa nyara na hawajapatikana, huku visa 69 vikiwa vimeripotiwa katika vituo vya polisi. Malawi inayo takriban walemavu wa ngozi 10,000 ambao wanaishi kwa woga kufuatia visa hivyo.

Ripoti hiyo ya Amnesy International yenye kichwa cha maneno sisi si wanyama kuwindwa au kuuzwa inaonyesha kuwa visa vya ukatili dhidi ya wanaoshi na ulemavu wa ngozi nchini Malawi vimeongezeka zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, huku watu wane akiwemo mtoto wakiuawa mwezi Aprili mwaka huu.Ripoti hiyo imevitwika lawama vyombo vya usalama nchini humo na hasa polisi kwamba imeshindwa kuzuia ongezeko la mauaji ya watu hao.

Hali ambayo imezidisha uwoga kwa familia zenye watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi. Afisa wa shirika la Amnesty International anayehusika na eneo la kusini ya Afrika Deprose Muchena amesema maafisa wa Malawi wameshindwa kuwalinda watu hao na hivyo kuwaacha katika hatari ya magenge ya wahalifu wanaowinda kuvinyofoa viungo vyao kwa imani potofu za kishirikina. Bi Edna anaeleza jinsi alivyopokonywa mtoto wake mmoja kati ya watoto wake pacha akishuhudia."Kundi la wanaume liliingia nyumbani baada ya kuvunja mlango, wakamshika mtoto mmoja kwa kichwa, name nikamshika miguu, tukawa tunavuta upande upande. Mtu mmoja akatoa kisu na kunikata mkono, ikabidi nimuachie na wakaenda na mtoto wangu. Hadi leo mwenzake huniuliza ndugu yangu yuko wapi."

Tanzania, Henry Mdimu.
Tanzania, Henry Mdimu.Picha: DW/A. Lattus

Ubaguzi dhidi ya walemavu wa ngozi

Visa hivyo vinachochewa na imani potofu kuwa viungo vyao huuziwa washirikina nchini humo na Msumbiji ili kufanya uganga wa kutafuta utajiri, bahati au kuondoa mikosi. Amnesty liinaamini kuwa idadi kamili ya walemavu wa ngozi ambao wameuawa iko juu zaidi, kufuatia kafara zinazofanywa kisiri bila ya kuripotiwa. Kadhalika hakuna orodha ya mara kwa mara kuhusu visa vinavyoripotiwa dhidi yao nchini Malawi.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa walemavu hao hukabiliwa na dhuluma tele, kutukanwa , kutengwa na kufanyiwa vitendo vya unyanyapaa katika jamii huku wengine wakifa kutokana na saratani ya ngozi kwa kukosa vifaa vya kujikinga dhidi ya miale ya jua inayowasababishia saratani. Overston Kodowe ambaye ni mwathiriwa anasema "Kuna imani nyingine kuwa hatuishi kwa miaka mingi, kwamba hatufariki na kuwa tunatoweka tu kimiujiza, hivyo hata waajiri wanachelea kutupa kazi kwa kuhofia tutatoweka tuache kazi."

Ilibainika kuwa jamaa za walemavu hao ni miongoni mwa wale wanaopanga njama za kuuawa kwa walemavu wa ngozi katika familia zao. Aidha kwa mujibu wa shirika la Amnesty hata maiti za walemavu wa ngozi zilizozikwa hufukuliwa kwa njia zisizohalali na maiti hizo kukatwa viungo. Polisi wamerekodi visa vya makaburi 39 yaliyofukuliwa.

Mwandishi: John Juma/Amnesty Report

Mhariri: Yusuf Saumu