1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimu wanaohusishwa na Ugaidi wafukuzwa kazi Uturuki

22 Novemba 2016

Uturuki imewafuta kazi walimu karibu elfu 28,000 na kuwasimamisha kazi wengine elfu 9,500 kwa madai ya kuhusika na ugaidi,wakati huo huo imetoa waranti wa kukamatwa kwa viongozi kadhaa wa Kikurd.

https://p.dw.com/p/2T4qO
Türkei Proteste
Picha: DW/D.Cupolo

Kauli hiyo imetolewa jana na naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, mpaka sasa Uturuki imeshawafukuza na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma wapatao 100,000 idadi hiyo ikijumuisha mahakimu, waendesha mashitaka, maafisa wa polisi na walimu tangu kikundi cha wanajeshi walipojaribu kuipindua Serikali. Viongozi wa Kikurd wanashutumiwa kuhusika na mlipuko wa bomu la kutegwa kwenye gari, mwezi Februari katika mji mkuu wa nchi hiyo Ankara na kuuwa watu 30.

Watu wapatao 40,000 wanashikiliwa na polisi wakishukiwa kuwa na mafungamano na Imam Fethullah Gulen, anayeishi nchini Marekani ambaye Serikali ya Ankara inamshutumu kuhusika na jaribio hilo. Gulen, ambaye alikimbia kuishi uhamishoni nchini Marekani tangu mwaka 1999 amekana kuhusika na kulaani tukio hilo.

Ukandamizaji huo umeibua wasiwasi kutoka kwa makundi ya haki za binadamu pamoja na washirika wa Magharibi wa nchi hiyo, wanahofia kuwa huenda Rais Tayyip Erdogan anatumia jaribio hilo lililoshindwa kama kisingizio cha kuwakandamiza wapinzani.

Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan
Raisi wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Picture-Alliance/dpa/S. Sunat

Walimu wengi kutoka jamii ya Kikurd kusini mashariki mwa Uturuki wamekuwa walengwa wakuu katika wiki za hivi karibuni, mamlaka zikiwatazama kama watu wenye mafungamano na chama cha wafanyakazi cha Kikurd PKK.

Hatua  zaidi kuendelea kuchukuliwa

Akizungumza baada ya cha kikao cha baraza la Mawaziri, naibu Waziri Mkuu Nurettin Canikli alisema kuwa karibu walimu 28,000 wameondolewa kutoka katika nafasi zao, na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea kwa wengine 9,500 ambao wamesimamishwa. Na kusema kuwa hatua stahiki lazima zichukuliwe kwa walimu pamoja na watumishi wengine wa umma wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na mashirika ya kigaidi.

Hivi karibuni kulifanyika maandamano kupinga hatua zinazochukuliwa na Serikali, Vedat Sevim ni mmoja kati ya waandamanaji, anasema nchi imegeuka kuwa sehemu mbaya kabisa, na kuna matatizo yasiyohesabika.

Naibu Waziri Mkuu huyo aliongeza kuwa, walimu wengine 455 ambao hapo awali waliondolewa kazini wamerejshwa baada ya uchunguzi kukamilika. Mara baada ya jaribio la Julai 15 mamlaka nchini Uturuki ilivifungia vyuo vikuu 15 na shule za sekondari 1,000 zenye uhusiano na Gulen, kufungwa kwa taasisi hizo kuliwaacha wanafunzi 200,000 wakiwa na wasiwasi kuhusu kuendelea na masomo hofu ikiwa ni hofu ya kupingwa mstari mweusi kwa shule za Gulen.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu