1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimwengu wakutana Tunis kuzungumzia Syria

24 Februari 2012

Wawakilishi wa mataifa ya magharibi na wa jumuiya ya nchi za kiarabu wanaohudhuria mkutano wa "Marafiki wa Syria" mjini Tunis wametoa mwito misaada ya kiutu iruhusiwe kuepekwa Syria

https://p.dw.com/p/149dT
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa marekani Hillary Clinton na wajumbe wengine katika mkutano wa "Marafiki wa Syria mjini TunisPicha: REUTERS

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka nchi zaidi ya 50 wanashiriki katika mkutano huo wa kwanza wa kimataifa katika mji mkuu wa Tunisia,Tunis,wakilenga kusaka ufumbuzi wa mzozo unaoendelea karibu mwaka mzima sasa nchini Syria.

Mswaada wa azimio uliolifikia shirika la habari la Uingereza Reuters, unasema wajumbe wanaitaka serikali ifungue njia ya kuingizwa misaada ya dharura katika miji ya Homs,Deraa,Zabadani na katika "maeneo mengine yanayokaliwa".Wajumbe wametoa mwito wa kusitishwa haraka matumizi ya nguvu.

Wameahidi kutoa misaada ya kiutu katika kipindi cha masaa 48 yajayo ikiwa Syria itaacha kuwashambulia raia na kuruhusu misaada hiyo iwafikie wale wanaoihitaji.

Kämpfe in Homs Syrien
Mapigano yanaendelea pia HomsPicha: AP

"Tumeingiwa na wasi wasi kuhusiana na kuongezeka mahitaji ya misaada ya kiutu nchini Syria" amesema msemaji wa shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu Hicham Hassan.

Mswaada huo wa azimio hazungumzii mataifa ya kigeni kuingilia kijeshi nchini Syria wala hauliangalii baraza la taifa nchini Syria kama mwakilishi pekee halali wa wananchi wa Syria,bali kama mwakilishi halali wa wasyria wanaodai mageuzi ya amani na ya kidemokrasi.

Wawakilishi wa baraza hilo la taifa-linaloyaleta pamoja baadhi ya makundi ya upinzani limetoa mwito wa kupatiwa silaha jeshi huru la Syria na makundi yote ya upinzani dhidi ya serikali ya Syria.Msemaji wa baraza hilo Ausama Monajed amesema:""Hilo linategemea uamuzi wa kisiasa.Pakifikiwa uamuzi wa kisiasa kutoka baraza la taifa la Syria na jumuia ya kimataifa kuupatia silaha upande wa upinzani, halitakuwa suala gumu.Hapo tutasaliwa na njia moja tu,nayo ni kupambana na vikosi vya Assad tukiwa na uongozi mmoja kwa lengo la kusonga mbele na kudhibiti ardhi nchini."

Syrien - Kämpfe - Homs
Vifaru vya jeshi la SyriaPicha: Reuters

Upande wa upinzani wa Syria unasema tayari wasyria wanaoishi uhamishoni wameanza kununua silaha na kuziingiza magendo nchini Syria kuwasaidia wapiganaji wa jeshi huru."Tayari tunaingiza silaha,kutoka kila mahala hata katika nchi za magharibi."amesema mwanaharakati mmoja wa upinzani ambae hakutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi Annan aliyechaguliwa kwa pamoja na Umoja wa mataifa na jumuiya ya nchi za kiarabu alishughulikie suala la Syria anatoa mwito wa kupatikana ufumbuzi wa amani.

Na nchini Syria kwenyewe mapigano yameripotiwa kuendelea Deraa hii leo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed