1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana dhidi ya sheria ya kumiliki silaha

Yusra Buwayhid
18 Februari 2018

Waathirika wa shambulio la risasi la hivi karibuni katika shule ya jimbo la Florida, Marekani wameandamana baada ya wanasiasa kushindwa kuchukua hatua kufuatia umwagaji damu wa mauaji ya watu 17.

https://p.dw.com/p/2sse0
USA Anti-Waffen-Demonstration in Fort Lauderdale
Picha: Reuters/J. Drake

Maelfu ya wanafunzi, wazazi na wanaharakati wanaopigania udhibiti wa bunduki nchini Marekani wameandamana Jumamosi katika mji wa jimbo la Florida wa Fort Lauderdale, wakidai mabadiliko ya sheria ya udhibiti wa bunduki, baada ya kijana mmoja kwa jina la Nikolas Cruz kuwaua watu 17 kwa kuwafyatulia risasi katika shule ya sekondari ya mji jirani wa Parkland.

Maandamano hayo yameibua hisia za kisiasa kutokana na gadhabu waliyonayo wananchi wanaomboleza tukio hilo lililosababisha umwagaji damu katika shule ya sekondari ya Marjory Stoneman Douglas.

Maafisa nchini humo wanasema kijana huyo mwanafunzi wa zamani ambaye alifukuzwa shule alikuwa na matatizo ya akili na vyombo vya usalama tayari vilifahamishwa. Maafisa wanasema alitumia bunduki aliyoinunua kwa kutumia njia halali za kisheria kutekeleza mauaji hayo.

"Kwa sababu ya sheria hizi za bunduki, watu ninaowajua, watu ninaowapenda, wamekufa, na sitawaona tena, "Delaney Tarr, mwanafunzi wa shule hiyo, aliuambia umati wa watu uliokusanyika nje ya mahakama ya Fort Lauderdale.

"Aibu kwenu," umati ulipiga mayowe.

Aidha wanafunzi hao wamemkosoa rais Donald Trump  pamoja na chama cha wamiliki wa bunduki nchini Marekani (NRA) kwa kuweka mazingira magumu ambapo  hoja inayohusiana na udhibiti wa bunduki imekuwa ikikumbana na upinzani mkali.

Laurie Woodward Garcia, mama wa mtoto wa miaka 14, amesema wengi wa watu walioandamana hapo wanaamini shambulizi hilo litapelekea kupatikana mabadiliko, lakini pia kuna wengi wasioamini hilo. "Kama kuna kitu cha kutuunganisha Wademocrat na Warepublican basi ni watoto wetu. Hivyo mabadiliko yatatokea," amesema Garcia.

Katika mji wa St. Petersburg, kwenye Ghuba la Florida ya maili 250 (maili 400) kaskazini magharibi mwa Parkland, mamia ya watu walikusanyika Jumamosi usiku katika bustani moja, ambapo waliwasha mishumaa kuwakumbuka waathirika na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha vurugu zinazotokana na umiliki wa bunduki.

USA - Florida Shooting - Trauer
Mkusanyiko wa kuwakumbuka waathirika wa shambulio la shule ya FloridaPicha: Reuters/J. Skipper

FBI yakiri makosa

Shirika la Upelelezi la nchini Marekani, FBI, limekiri kupokea taarifa mara mbili tofauti juu ya Cruz, lakini lilishindwa kuchukua hatua za mapema. Taarifa moja waliipata mwezi Septemba, pale mtu mmoja aliporipoti ujumbe wa kushtua ulioachwa katika ukurasa wake wa mtanado wa Youtube na mtu anaejulikana kwa jina la Nikolas Cruz. "Nitakuwa mtaalamu wa kufyatua risasi katika shule," ulisema ujumbe huo. Shirika la FBI hata hivyo halikuweza kuthibitisha chanzo cha ujumbe huo.

Baada ya hapo, mwezi Januari, mtu wa karibu na Cruz alilipigia simu shirika la FBI akiwa na taarifa juu ya Cruz kumiliki silaha na kuonyesha tabia zisizo za kawaida, lakini shirika hilo lilishindwa kufuatilia taarifa hizo.

Shirika la FBI limekiri kwamba taarifa hiyo ilifaa kutumwa katika ofisi zake za Miami, ambako ingeweza kufanyiwa uchunguzi zaidi. Liwali wa kaunti ya Broward, Scott Israel, amesema ofisi yake pia imepokea zaidi ya taarifa 20 kwa njia ya simu zinazomhusu Cruz katika miaka michache iliyopita.  Takriban simu mbili kati ya hizo zilipigwa na mama yake mzazi, kabla ya kifo chake mwezi Novemba.

Shuleni, Cruz ameelezwa kuwa akipigana na walimu mara kwa mara, amewahi kushitakiwa kwa kuwatukana wafanyakazi wa shule na aliwahi kufanyiwa "tathmini ya mtu wa kitisho". Rekodi zinaonyesha kwamba alifukuzwa kwa muda shuleni mara kadhaa kati ya mwaka 2016-2017 na mara nyingi hakuhudhuria shule. Rekodi pia zinaonyesha kwamba Cruz alisoma katika shule sita tofauti ikiwa ni pamoja na shule ya wanafunzi wenye matatizo za kihisia.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dw/ap

Mhariri: Isaac Gamba.