1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani wavutana kujinusuru na madeni.

27 Julai 2011

Ikiwa imebaki siku chache tu kabla ya Agosti mbili ,muda uliowekwa wa kupatikana maafikano ya kuongeza kiwango cha mkopo, ambacho serikali inaweza kupata. viongozi nchini humo wamegawanyika kupata ufumbuzi.

https://p.dw.com/p/124wP
Rais Obama akiwa na spika wa Baraza la wawakilishi John BoehnerPicha: dapd

Viongozi na wabunge kutoka chama tawala cha Democratic na chama cha upinzani cha Republican wamegawika katika kupigania kufikia msimamo wa pamoja,huku Rais Barack Obama ametishia kutumia mamlaka aliyonayo kupinga mpango wa chama cha upinzani. 

Mpango wa chama hicho cha upinzani nchini Marekani cha Republican kupunguza nakisi, leo unatarajiwa kukakabiliwa na upinzani mkali na pia kucheleweshwa, hali inayozua wasiwasi miongoni mwa wawekezaji na raia wa kawaida wa Marekani, ambao wanatumaini ya kupatikana muafaka katika dakika za mwisho kabla ya kufikia Agosti mbili, ili kuepusha mgogoro wa madeni.

Mgawanyo mkubwa kati ya viongozi wa Republican na Democrat katika kupigania kupata msimamo wa pamoja ikiwa zimesalia siku kidogo kabla ya  muda  ambapo bunge linatakiwa kuupitisha. Bila ya kufanya hivyo serikali ya Marekani  itafilisika. Hali ambayo mgogoro huo wa madeni unaweza kusambaratisha masoko ya kimataifa.

Vyama hivyo vya Republican na Democrat vimekuwa vikijizatiti kila kimoja katika matakwa yake muhimu na kulaumiana kila upande kuweka mbele masuala ya kisiasa katika maslahi ya taifa. Huku nafasi ya kupatikana ufumbuzi wa haraka ikiwa ndogo baada ya kura juu ya mpango wa nakisi wa chama cha Republican ambao ulikuwa uwasilishwe leo bungeni kusogezwa mpaka kesho.

Spika  wa baraza la wawakilishi wakutoka chama cha Republican John Boehner aliharakisha  kufanyia marekebisho muswada wake baada ya uchunguzi kugundua kwamba muswada huo utapunguza matumizi kwa dola bilioni 350 kiwango ambacho ni chini ya kile cha dola trilioni 1.2 alichodai kupendekeza kwa zaidi ya miaka 10.

Hata hivyo Rais Barack Obama ametishia kutumia mamlaka yake kupinga mpango huo wa Boehner , huku spika wa baraza la Senete Harry Reid kutoka chama cha Democrats akiutaja  mpango huo wakati ukiwaslishwa , kuwa umekufa.

Mpango huo pia umeshindwa kuungwa mkono na wanachama wahafidhina wa Republican wa kundi linalojiita "Tea Party", ambao wamekataa kuunga mkono kuongezeka kwa kodi na ambao wanataka kupunguzwa kwa kiasi kikubwa katika mipango ya jamii ambayo imekuwa ikikingiwa kifua na chama cha Rais Obama cha Democrat.

Ikulu ya Marekani ilisema jana kwamba inafanyakazi pamoja na bunge la nchi hiyo ili kutafuta mpango mbadala wa kuweka matumaini ya kwamba muwafaka unaweeza kupatikana katika muda wa mwisho wakati wabunge wakizidi kukumbwa na shinikizo kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi katika masoko ya fedha.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed