1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi huo utafanyika kwa awamu mbili

18 Oktoba 2015

Wamisri wanapiga kura leo Jumapili(18.10.2015)kulichagua bunge linalotarajiwa kumuunga mkono rais Abdel Fattah al-Sisi, ambaye amezima upinzani wote tangu kumuondoa madarakani mtangulizi wake mwaka 2013.

https://p.dw.com/p/1GpwU
Ägypten Parlamentswahl 2015
Uchaguzi wa bunge 2015 nchini MisriPicha: picture-alliance/dpa/K. Elfiqi

Uchaguzi huo ambao umecheleweshwa mno kwa ajili ya kulichagua bunge lenye wabunge 596--bunge lililopita limevunjwa Juni 2012--utafanyika kwa awamu mbili kati ya Oktoba 17 na Desemba 2.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa tatu asubuhi saa za Misri hadi saa tatu usiku, ambapo zaidi ya watu milioni 27 katika majimbo 14 kati ya 27 nchini Misri wakiwa na haki ya kupiga kura leo Jumapili (18.10.2015) na kesho Jumatatu(19.10.2015) katika awamu ya kwanza ya uchaguzi.

Ägypten Parlamentswahl 2015
Mabango ya uchaguzi mjini CairoPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Nabil

Uungwaji mkono Sisi

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema wengi wa wagombea zaidi ya 5,000 katika uchaguzi huo wanamuunga mkono kwa kiasi kikubwa Sisi na wanatarajiwa kudhibiti bunge.

"Iwapo wabunge watataka, wataweza aina fulani ya uwiano," amesema Youssri al-Azabawi, mtaalamu katika kituo cha Ahram kwa ajili ya mitaala ya kisiasa na mikakati.

"Lakini , kutokana na umashuhuri wa Sisi, hilo halitatokea. Rais atabakia na madaraka makubwa."

Wamisri wengi wamechoshwa na vurugu za kisiasa tangu mwaka 2011 alipoondolewa madarakani rais wa siku nyingi Hosni Mubarak, wanamuunga mkono Sisi, ambaye ameapa kuufufua uchumi wa Misri unaoyumba na kurejesha uthabiti kwa kutumia ukandamizaji mkubwa ambapo umewalenga waungaji mkono mtangulizi wa rais Mubarak, Mohammed Mursi.

Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-SisiPicha: picture-alliance/dpa

"Ni bunge la kweli ambalo halitarajiwi kuwa la kimapinduzi ama la kufanya mabadiliko," amesema mchambuzi wa masuala ya kisiasa Hazem Hosni.

Wabunge kutokuwa na imani na rais

Katiba inalipa bunge uwezo wa kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na rais na pia inawapa wabunge siku 15 kuchunguze amri zote atakazotoa rais.

Lakini uchaguzi huo unaofanyika bila ya upinzani wa kweli na haujaleta hamasa kubwa katika uchaguzi wa kwanza tangu baada ya kuondolewa rais Mubarak madarakani mwaka 2011.

Kundi la Udugu wa Kiislamu ambalo limekuwa na wabunge wengi katika bunge lililopita limepigwa marufuku, wakati makundi ya mrengo wa shoto na yale yenye msimamo usioelemea katika dini ambayo yameongoza vuguvugu la mwaka 2011 yanasusia uchaguzi huo ama hayana uwakilishi wa kutosha katika uchaguzi huo.

Wakati Wamisri nje ya nchi hiyo wakianza kupiga kura jana Jumamosi (17.10.2015), rais alijitokeza katika televisheni akitoa wito kwa wananchi kupiga kura.

Symbolbild Ägypten Kairo Vergewaltigung auf dem Tahrir-Platz
Ukandamizaji wa serikali dhidi ya kundi la Udugu wa Kiislamu nchini MisriPicha: Reuters

"Furahieni fursa ya uwakilishi na kufanya maamuzi sahihi," amesema kiongozi huyo wa zamani wa jeshi.

"Natarajia vijana wa Misri kuwa nguvu inayowezua kutusukuma mbele katika sherehe hizi za demokrasia."

Wakati akiwa bado mkuu wa jeshi , Sisi alimuondoa maradakani Mohammed Mursi -- rais aliyechaguliwa kwa njia huru -- Julia mwaka 2013 baada ya maandamano makubwa ya umma dhidi ya utawala wake uliodumu kwa mwaka mmoja uliokuwa unaleta mtengano.

Ukandamizaji wa serikali

Ukandamizaji wa serikali iliyochukua nafasi yake uliwalenga wafuasia wa Mursi wa kundi la Udugu wa Kiislamu-- ambao ulishinda chaguzi zote tangu kuangushwa kwa Mubarak mwaka 2011 -- na kushuhudia watu 1,400 wakiuwawa na mamia kwa maelfu wakitupwa jela.

Mamia ikiwa ni pamoja na Mursi binafsi wamehukumiwa kifo baada ya kesi ya halaiki ambapo Umoja wa mataifa umeshutumu kuwa "kitu kisichohitajika katika historia ya hivi karibuni".

Ägypten Journalisten Protest Archiv 2012
Uhuru wa kujieleza unakandamizwa nchini MisriPicha: picture alliance/AP Photo

Kundi la Udugu wa Kiislamu hivi sasa limewekwa katika orodha ya "kundi la kigaidi" na wanachama wake wamepigwa marufuku kugombea uchaguzi.

Sisi wakati huo huo , ameshinda uchaguzi wa rais mwaka 2014.

Polisi kadhaa na wanajeshi wameuwawa katika mashambulizi ya makundi ya jihad tangu ukandamizaji huo dhidi ya watu wanaofuata itikadi kali ya dini ya Kiislamu kuanza.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buawayhid