1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri wapiga kura kuchagua rais

23 Mei 2012

Maelfu ya Wamisri wamemiminika vituoni kupiga kura ya kumchagua raisi wao ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuondoka madarakani kwa Hosni Mubarak mwanzoni mwa mwaka jana.

https://p.dw.com/p/150Pi
Mpigakura akitumbukiza kura yake kwenye kisanduku katika uchaguzi wa Jumatano, 23 Mei 2012.
Mpigakura akitumbukiza kura yake kwenye kisanduku katika uchaguzi wa Jumatano, 23 Mei 2012.Picha: Reuters

"Ninaweza kufa miezi michache tu ijayo, hivyo nimekuja kupiga kura kwa ajili ya wangu, ili wao waweze kuishi," Med-hat Ibrahim, mtu mzima wa miaka 58, ambaye anauguwa ugonjwa wa saratani, ameliambia shirika la habari la AFP akiwa kwenye mstari wa kupiga kura katika viunga masikini vya jiji la Cairo. Akibubujikwa na machozi, Ibrahim amesema Wamisri wanataka kuishi maisha bora kama wanaadamu.

Wagombea kumi na tatu wakiwamo wa vyama vyenye kuegemea Uislamu, waliberali na hata waliohudumu kwenye utawala wa Mubarak, wanagombea uchaguzi huu wa leo. Hata hivyo, hakuna mgombea anayetegemewa kupata ushindi wa moja kwa moja katika uchaguzi huu wa siku mbili, na hivyo duru ya pili inatarajiwa kati ya wagombea wawili watakaopata nafasi za juu, hapo Juni 16 na 17.

Ziyad Alimi, mbunge wa chama cha Kisoshalisti, anasema kwamba kura hii inapaswa kuamua hatima ya kweli na ya kudumu ya Wamisri, na sio kuiondoa nchi kwenye udikteta wa kundi moja na kuiweka kwa wa kundi jengine

Wapiga kura wakiwa katika mstari kwa ajili ya kupiga kura zao kwenye uchaguzi wa rais wa Misri.
Wapiga kura wakiwa katika mstari kwa ajili ya kupiga kura zao kwenye uchaguzi wa rais wa Misri.Picha: Reuters

"Leo watu wanapiga kura kumpata raisi atakayewaongoza, ambaye bila ya kuwa naye, Katiba yetu itakuwa haina maana. Tutakuwa na rais ambaye madaraka yake hayako wazi."

Kwa miaka 29 ya utawala wake, Mubarak, kama walivyokuwa watangulizi wake, aliendesha kura za maoni za ndiyo ama hapana kwa nafasi ya uraisi. Hata uchaguzi wa 2005, ambapo Mubarak alikubali kuwa na washindani kwa kiti cha uraisi, ulimalizika sio tu kwa ushindi mkubwa upande wake, bali pia kifungo cha jela kwa wapinzani wake. Uchaguzi wa bunge uliokuwa ukifanyika, ulimalizika kwa ushindi mkubwa wa chama tawala, huku kukiwa na matukio kadhaa ya wizi na udanganyifu wa kura.

Rais ajaye wa Misri atakuwa wa tano kwa taifa hilo tangu mapinduzi ya mwaka 1952 yaliyouondoa utawala wa kifalme, na kuliingiza kwenye uongozi wa kijeshi kwa karibuni miongo sita. Kama walivyokuwa watangulizi wake, Anwar Saadat, Gamal Abdel-Nasser na Mohammed Naguib, Mubarak naye alitokea kwenye jeshi.

Suala kuu lililoongoza kampeni za urais kwenye uchaguzi huu, lilikuwa ni siasa za Mashariki ya Kati, ambapo hoja ya kufanyiwa marekebisho kwa mkataba wa amani wa mwaka 1979 kati ya Misri na Israel, ilitawala. Inaripotiwa kuwa bado Wamisri wengi wanaichukulia Israel kuwa adui yao mkubwa.

Wanajeshi wakimsaidia mama mmoja kuondoka kituoni baada ya kupiga kura.
Wanajeshi wakimsaidia mama mmoja kuondoka kituoni baada ya kupiga kura.Picha: Reuters

Japokuwa hakuna mgombea hata mmoja aliyeonesha nia ya kujitoa kwenye mkataba huo, lakini ushindi wa mgombea yeyote wa vyama vya Kiislamu au vya mrengo wa kushoto, utamaanisha kulegea kwa mahusiano na Israel na kuimarika kwa uungwaji mkono kwa Wapalestina katika utaratibu wa kupatikana amani kwenye Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman