1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachama wawili wa upinzani waachiwa huru Syria

Admin.WagnerD31 Desemba 2015

Serikali ya Syria imewaachilia huru wanachama wawili mashuhuri wa upinzani ambao walikuwa wamekamatwa Jumatano wakati wakiwa safarini kuelekea Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia kukutana na wapinzani wengine wa serikali.

https://p.dw.com/p/1HWTK
Mji wa Holms kufuatia mashambulizi ya serikali.
Mji wa Holms kufuatia mashambulizi ya serikali.Picha: Reuters/Sana

Ahmed al Asrawi na Munir al-Bitar wa Kamati ya Uratibu ya Taifa inayopigania Mabadiliko ya Kidemokrasia nchini Syria walizuiliwa kwenye mpaka wa Syria na Lebanone nwakati walipokuwa wakielekea Saudi Arabia kukutana na wanachama wenzao wa upinzani wanaounda kamati kuu ya mazungumzo ya kutafuta usuluhishi kwa mzozo wa Syria.

Katibu Mkuu wa kamati hiyo Yahya Aziz ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanachama hao wawili walipokamatwa walipelekwa mahala kusikojulikana na kwamba watu wanaotaka usuluhishi wa kisiasa wasingelifanya jambo hilo.

Kamati hiyo ya wanachama 33 imeundwa hapo mwezi wa Disemba katika mkutano wa kihistoria uliofanyika Riyadh wa makundi ya wapiganaji na wapinzani wa kisiasa.

Kamati hiyo ilikuwa inapanga kuchaguwa sehemu ya ujumbe wa upinzani kwa ajili ya mazungumzo ya amani na serikali ya Bashar al -Assad yaliopangwa kufanyika mwezi ujao.

Syria na wasirika wake zalaumiwa

Kamati hiyo ya uratibu ya taifa kwa ajili ya mabadiliko ya demokrasia nchini Syria baadae imetangaza katika mtandao wake wa Facebook kuachiliwa kwa wenzao hao al Asrawi na Munir na kutowa wito wa kuachiliwa kwa wafungwa wengine wote na mahabusu.

Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Rais Bashar al-Assad wa Syria.Picha: picture-alliance/dpa/ Sana/Handout

Hapo awali kundi hilo limesema kukamatwa kwao kunakiuka juhudi za kimataifa kufikia suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Syria.Taarifa kutoka kwa kamati hiyo imesema wanachama hao walikuwa wakitazamiwa kukutana na viongozi wengine wa upinzani hapo Januari Mosi kukamilisha uteuzi wa ujmbe utakaouzungumza na serikali.

Taarifa yao hiyo imeendelea kusema kwamba serikali ya Syria na washirika wake wa Iran na Urusi hawako makini kuhusu mchakato wa kisiasa kwa sababu wanawaandama wanachama wa mkutano huo wa Riyadh ambao wamejitolea kutafuta suluhisho la kisiasa.

Kukamatwa kwao kunakuja katika kipindi kisichozidi wiki moja baada ya jeshi la Syria kudai kuhusika na mauaji ya kiongozi wa upinzani Zahran Alloush.

Mapambano yaendelea

Waasi hapo jana wameshambuliana kwa risasi na vikosi vya serikali katika mji wa Sheikh Maskin. Jeshi la Syrima limesema limeweza kuingia katika mji huo unaoshikiliwa na waasi hapo Jumanne.Mji huo uko kwenye njia kuu ya kusafirisha mahitaji kutoka mji mkuu Damascus na kukatiza katika jimbo la kusini la Deraa.

Mwanajeshi wa kikosi cha serikali.
Mwanajeshi wa kikosi cha serikali.Picha: Getty Images/AFP/Str

Miripuko miwili ya mabomu imeuwa watu 17 na kujeruhi wengine themanini katika mji wa kaskazini mashariki wa Qamishi unaokaliwa na wakaazi wengi wa Kikurdi.

Shirika la habari la Syria SANA limesema miripuko hiyo imetokea Jumatano usiku katika eneo la Shiyahi mjini humo ambacho ni kitongoji kinachokaliwa na Wakristo.

Kundi la Uangalizi wa Haki za Binadamu nchini Syria limesema mabomu hayo yameripuliwa katika mikahawa miwili katikati ya mji karibu na kituo cha ukaguzi wa usalama kinachosimamiwa na vikosi vya serikali.

Kundi la Dola la Kiislamu limekuwa likipambana na wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria tokea mwaka jana wanamgambo hao wa itikadi kali wamefanya mashambulizi kadhaa ya kujitowa muhanga dhidi ya Wakurdi mengine katika mji huo wa Qamishi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman