1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanadamu wote wako huru na ni sawa

15 Juni 2011

Wakati dhana ya utandawazi ilichukuliwa na wengi kuwa ni ahadi ya maisha mema, haki za binaadamu zimejikuta zikiwa hatarini kutokana na sababu kadhaa zinazohusiana kwa njia moja au nyengine na dhana hii.

https://p.dw.com/p/11YG6
Haki za binaadamu zinazidi kuvunjwa ulimwenguni
Haki za binaadamu zinazidi kuvunjwa ulimwenguni

Maendeleo, teknolojia, mtandao wa intaneti na nguvu za masoko ni mambo yaliyopaswa kuyafanya matarajio ya watu kutoka pande zote za ulimwengu na mataifa yote kutimia.

Na sababu ni kuwa wanaadamu wote wamezaliwa wakiwa na uhuru, heshima na haki sawa. Ndivyo kinavyosema Kifungu cha 1 cha Tamko la Haki za Binaadamu la Ulimwengu.

Lakini katika siku za karibuni kumekuwa na hali ya kupotea njia kwa ulimwengu. Kwa upande mmoja, mataifa makubwa yanaingia kwenye migogoro, hasa kwa sababu ya masoko ya kifedha, na, kwa upande mwengine, majanga ya kimazingira yameanza. Maji, ardhi na rasilimali nyengine muhimu kwa mataifa yanayoendelea zinazidi kunyang'anyiwa.

Maonesho ya picha juu ya haki za binaadamu ya Muirani, Pantea Bahrami
Maonesho ya picha juu ya haki za binaadamu ya Muirani, Pantea BahramiPicha: Pantea Bahrami

Badala ya kuwaendeleza watu katika nchi hizo masikini, rasilimali hizi zinakuwa chanzo cha kuyachafua maeneo mengi ziliko, huku zikisababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Watu wanaishi katika hali ya mashaka na tabu, huku wakijikuta wametengwa na mfumo wa dunia. Ni wapweke na wamepoteza matumaini.

Watu hawa wanatafuta na wanahitaji ushirikiano na mshikamano wa kila mmoja wetu katika kuwa na maisha yenye muelekeo: kazi yenye heshima, makaazi ya kibinaadamu.

Haya ni mambo ambayo kila mwanaadamu anatakiwa aahidiwe kupitia msaada wa kilimwengu, ambao hadi sasa unakosekana. Tamko la Kilimwengu la Haki za Binaadamu la mwaka 1948 linasisitiza zaidi juu ya haki za kiraia na za kisiasa kuliko haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.

Masuala yanayohusu hali za maisha na hali ya kutokuwepo ubaguzi kwenye soko la kazi na elimu, ni mambo ya msingi katika haki za binaadamu. Mwaka 1966, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha tamko la kuzitambua haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni na mwaka 1976 zikafanywa kuwa sehemu ya Tamko la Haki za Binaadamu la Ulimwengu. Mataifa 160 yameweka saini, na hivyo kuahidi kuhakikisha raia wao wanapata haki hizi.

Mwandishi: Ulrike Mast-Kirschning
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji