1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati yafanyika Paris

15 Januari 2017

Ufaransa imeonya kuzuka "madhara mabaya" iwapo Donald Trump atachukuwa hatua ya kuutambuwa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel huku wawakilishi kutoka nchi 70 wakikutana Paris kufufuwa mazungumzo ya amani yaliokwama.

https://p.dw.com/p/2VpyC
Frankreich Paris Nahost Friedenskonferenz Gruppenfoto
Picha: Reuters/B. Guay

Israel na Wapalestina hawakuwakilishwa katika mkutano huo wa Jumapili (15.01.2017) ambao Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameuupuzilia mbali kuwa hauna tija.

Akifunguwa mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema jumuiya ya kimataifa inataka "kusisitiza kwa nguvu kwamba suluhisho la mataifa mawili ni ufumbuzi pekee unaowezekana" kwa mzozo huo uliodumu kwa miongo saba.

Pia amemuonya rais huyo mteule wa Marekani kuuhamishia ubalozi wa Marekani Jerusalem kutoka Tel Aviv katika hatua ya kuutambuwa mji huo unaozozaniwa kuwa mji mkuu wa Israel.

Madhara mabaya

Paris internationale Nahost-Konferenz
Wasziri wa msmbo ya nje wa Ufaransa Jean- Marc Ayrault na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.Picha: Getty Images/AFP/B. Guay

Ayrault amesema hatua hiyo ilioahidiwa kutekelezwa na Trump wakati wa kampeni itakuwa na "madhara mabaya sana " na ametabiri kiongozi huyo ajaye wa Marekani itamuia vigumu kuitekeleza.

Amekiambia kituo cha Televisheni cha Ufransa cha 3 TV "Unapokuwa rais wa Marekani huwezi kuchukuwa msimamo huo wa ukaidi na msimano wa upande mmoja katika suala hilo.Inabidi ujaribu kuweka mazingira kwa ajili ya amani."

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter-Steinmeier ameonya kwamba kuna hatari ya kupamba moto upya kwa mzozo huo huko Mashariki ya Kati kutokana na nia ya Trump kuhamishia ubalozi wa Mrekani Jerusalem.

Amesema jambo hilo linapaswa kuepukwa na kwamba mkutano huo unaweza kuchangia ambapo kwayo wale wote wenye utashi na amani ya kudumu Mashariki ya Kati wanakubali hilo na kuelezea ufumbuzi wa mataifa mawili ni njia pekee ya kusonga mbele.

Netanyahu na rais  wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas wamealikwa kukutana na Rais Francois Hollande kujadili hitimisho la mkutano huo.

Hauna tija

Frankreich Nahost-Konferenz in Paris
Mkutano wa Paris wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati .Picha: picture-alliance/abaca/C. Ozdel

Abbas ambaye ameunga mkono mkutano huo anategemewa kwenda Paris wiki chache zijazo lakini Netanyahu amekataa mwaliko huo kwa mujibu wa wanadiplomasia wa Ufaransa.

Waziri Mkuu wa Israel hapo Jumapili ameushutumu tena mkutano huo kwa kusema hauna maana.

Ameuambia mkutano wa mawaziri wa kila wiki "Mkutano huo umeratibiwa kati ya Ufaransa na Wapalestina kwa lengo la kuiwekea masharti Israel ambayo hayaendani na mahitajji yetu ya taifa."

Mkutano huo wa Paris kwa kiasi kikubwa ni wa ishara lakini unakuja katika wakati muhimu kwa Mashariki ya Kati siku tano kabla ya Trump kuapishwa kama rais wa Marekani.

Kuitumikia amani

Paris internationale Nahost-Konferenz
Waziri wa mabo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault na mwenzake wa Saudi Arabia Adel Al Jubeir.Picha: Reuters/T. Samson

Israel ambayo inasisitiza kwamba ni mazungumzo tu ya moja kwa moja na Wapalestina yanaweza kuleta amani kwa Mashariki ya Kati ina hofu kwamba mkutano huo unaweza kuja na hatua ambazo zinaweza kuwasilishwa Baraza lsa Usalama kabla ya Trump kuingia madarakani.

Ufaransa imesisitiza kwamba haina mipango hiyo.

Ayrault amesema "Ufaransa haina shauku nyengine isipokuwa kiutumikia amani na hakuna wakati wa kupoteza."

Mvutano kati ya Waisrael na Wapalestina umezidi kuongezeka kufuatia wimbi la mashambulizi ya Wapalestina.Israel kuendelea kutanuwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina wanayotaka kuunda taifa lao pia inaonekana kuwa kikwazo kikuu cha kupata suluhisho.

Juhudi hizo za kutafuta amani zimekwama tokea juhudi zilizoongozwa na Marekani kusambaratika hapo mwezi wa April mwaka 2014.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : John Juma