1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanadiplomasia wawili watimuliwa Afghanistan

27 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cgtn

KABUL.Wanadiplomasia wawili wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya waliyoko nchini Afghanistan wametimuliwa nchini humo baada ya kutuhumiwa kuwa na mahusiano na kundi la Taliban.

Maafisa hao ambao mmoja ni muingereza aliyekuwa akiwakilisha Umoja wa Mataifa na mwengine raia wa Ireland akifanyakazi Umoja wa Ulaya, wamekwishaondoka nchini humo.

Serikali ya Afghanistan inawatuhumu wanadiplomasia hao kuwa walikutana na viongozi wa kundi la Taliban bila ya ridhaa ya serikali hiyo.

Lakini kwa upande wake Umoja wa Mataifa umesema kuwa hatua hiyo ni sintofahamu iliyojitokeza kufuatia ziara ya wanadiplomasia hao na kwamba hivi sasa wanajadiliana na serikali ya Afghanistan juu ya suala hilo.

Wakati huo huo Rais Nicolaus Sarkozy wa Ufaransa ameondoka nchini Afghanistan kuelekea Tajikistan baada ya ziara yake ya kushtukiza ambako alikuwa na mazungumzo na Rais Hamid Karzai.

Kiongozi huyo wa Ufaransa pia alikutana na kikosi cha Ufaransa kilichoko kwenye jeshi la NATO nchini Afghanistan.

Katika mazungumzo yake na Rais Karzai, Rais Sakozy amesema kuwa jumuifa ya kimataifa haitakuwa tayari kushindwa kupambana na ugaidi nchini Afghanistan.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu mpya wa Australia Kevin Rudd naye amefanya ziara ya kushtukiza nchini Afghnaistan ambapo alikutana na kiongozi wa nchi hiyo Hamid Karzai.