1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati waiondoa kesi dhidi ya Uhuru, Ruto

29 Novemba 2012

Kesi iliyokuwa iamuwe iwapo Uhuru Kenyataa na William Ruto wanaoshukiwa kwa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya, wanaweza kugombea urais kwenye uchaguzi wa Machi 2013 imefutwa na mahakama.

https://p.dw.com/p/16sRQ
Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.Picha: dapd

Mashirika ya kiraia yaliyowasilisha shauri la kuwazuia Kenyatta na Ruto kugombea urais, yaliwaambia majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo kuwa swala la uadilifu katika kesi hiyo hauwezi kufikiwa iwapo wagombea wengine wa urais hawatajumuishwa katika kesi na hivyo wameamua kuiondoa kesi yao mahakamani.

Wanaharakati wa mashirika hayo wamesema hatua yao ya kuiondoa kesi hiyo ni njia moja ya kuipeleka tena mahakamani kwa kuwazingatia wanasiasa wote wanaowania urais. Wanasema hatua hiyo italipatia ufumbuzi swala la uadilifu.

Majaji hao Isaac Lenaola, Mohammed Warsame na Philomena Mwilu waliokuwa wasikilize kesi hiyo hii leo, walikubali hatua ya wanaharakati kuiondoa kesi wakisema wana haki kikatiba kufanya hivyo.

Kenyatta na Ruto waendelea na kampeni

Kenyatta ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa Kenya na Ruto ambaye ni mbunge wa Eldoret Kaskazini kwa sasa wanaendelea na kampeni zao za kuwania kiti cha urais nchini humo utakaofanyika mwezi Machi 2013.

William Samoei Ruto
William Samoei RutoPicha: AP

Kenyatta na Ruto wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2007 na 2008 zilizosababisha watu zaidi ya 1,000 kuuwawa na wengine 650,000 wakiachwa bila makaazi.

Wanasiasa hao wawili wanapaswa kujibu mashitaka hayo Aprili 2013, katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) The Hague, Uholanzi.

Tayari Kenyatta na Ruto wanajadiliana jinsi ya kuunda muungano wa kisiasa watakaotumia kugombea uongozi wa nchi. Wanasema wameamua kuunda muungano watakaoutumia kuwania nafasi ya rais na makamu wake katika uchaguzi mkuu mwaka ujao kama ishara ya kuwapatanisha Wakenya.

Mkutano wao wa pamoja unatarajiwa kufanyika Jumamosi mjini Nakuru eneo lililoathirika sana kutokana ghasia za baada ya uchaguzi wa Disemba 2007.

Mwandishi: Amina Abubakar
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman