1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 13 wauawa katika shambulizi Uturuki

Grace Kabogo
17 Desemba 2016

Wanajeshi 13 wa Uturuki wameuawa na wengine 48 wamejeruhiwa, baada ya basi lao kushambuliwa katika mji wa Kayseri, huku taarifa ya jeshi ikisema kuwa raia pia ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa.

https://p.dw.com/p/2USSw
Türkei Bus Explosion Kayseri
Picha: picture-alliance/AP Photo

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Suleyman Soylu, amesema kwa ujumla kiasi ya watu 55 wamejeruhiwa na 12 kati yao wako katika kitengo maalumu cha kuwaangalia wagonjwa, huku sita wakiwa mahututi. Gavana wa Jimbo la Kayseri, Suleyman Kamci amelielezea shambulizi hilo kama la kigaidi, akisema mshambuliaji aliyejitoa muhanga, aliripua mabomu yaliyokuwa kwenye gari.

Shambulizi hilo limetokea leo karibu na Chuo Kikuu cha Erciyes, kwenye mji huo uliopo katikakati mwa Uturuki. Basi hilo lilikuwa limewabeba wanajeshi waliokuwa wamemaliza kufanya doria, pamoja na raia. Basi hilo lilikuwa limesimama katika taa za kuongozea magari barabarani, wakati liliposhambuliwa na gari lililokuwa na mabomu.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amewalaumu wapiganaji wa Kikurdi kwa kuhusika na shambulizi hilo. Shambulizili hilo limefanyika wiki moja baada ya kutokea mashambulizi mengine mawili ya mabomu yaliyowalenga polisi mjini Istanbul.

Türkei  Kayseri Explosion Bus
Watu wakitoa msaada baada ya basi kushambuliwaPicha: Reuters/T.Bulut

Uturuki imekumbwa na mashambulizi kadhaa mwaka huu, huku wapiganaji wa Kikurdi na wale wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS, wakikiri kuhusika na mengi ya mashambulizi hayo.

Taarifa iliyotolewa na Rais Erdogan imeeleza kuwa aina na malengo ya mashambulizi haya yanaonyesha wazi nia ya kundi la magaidi wenye itikadi kali, ni kutaka kuivuruga Uturuki na kuiweka katika hali ya taharuki.

Polisi inawashikilia watu saba

Waziri Soylu, amesema hadi sasa polisi inawashikilia watu saba na wengine watano wanaendelea kutafutwa wakihusishwa na shambulizi hilo. Akizungumza katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Afya, Recep Akdag na waandishi wa habari, Soylu amethibitisha kuwa idadi ya waliojeruhiwa imeongezeka na kufikia 56. Aidha, Waziri Akdag amesema idadi kubwa ya ya watu wamepata majeraha madogo madogo.

Türkei Weltenergiekongress 2016 in Istanbul - Putin und Erdogan
Rais Vladmir Putin na Rais Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/A. Druzhinin

Hayo yanajiri wakati ambapo Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki, Numan Kurtulmus amesema mabomu yaliyotumika katika shambulizi la leo, yanafanana na yale yaliyotumika katika mashambulizi mawili ya mabomu wiki iliyopita mjini Istanbul. Kauli hiyo ameitoa wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cga NTV.

Wakati huo huo, Rais wa Urusi, Vladmir Putin amemwambia Rais Erdogan kuwa Urusi iko tayari kuongeza ushirikiano wake dhidi ya ugaidi. Kauli hiyo ameitoa kufuatia shambulizi la leo kwenye basi ambalo limewauwa wanajeshi.

Mashirika ya habari ya Urusi yameripoti kuwa Putin pia amemtumia Erdogan salamu za rambirambi kutokana na mauaji hayo na amesema ana uhakika kuwa jinsi ya kukabiliana na mashambulizi kama hayo ni kuongeza mapambano dhidi ya makundi yenye itikadi kali.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, DPA, AFP
Mhariri: Sudi Mnette