1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 3,000 zaidi wahitajika Jamhuri ya Afrika ya Kati

21 Februari 2014

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameiomba Jumuiya ya kimataifa kupeleka wanajeshi wengine 3,000 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi pale kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kitakapoundwa

https://p.dw.com/p/1BDAc
Picha: Reuters/Mark Garten

Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameliambia baraza la usalama la Umoja huo kuwa ataripoti kwa baraza hilo hivi karibuni mapendekezo ya kuundwa kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kitakachokuwa na mamlaka zaidi ya kulinda raia na kuimarisha uthabiti kwa taifa hilo ambalo hapo zamani lilitawaliwa na Ufaransa.

Ban amesema anatiwa wasiwasi mkubwa sana na ghasia katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo zinaonekana kuchukua mkondo wa kuwa mauaji ya halaiki na kutishia kuigawanya nchi hiyo vipande viwili.

Kiasi ya watu elfu mbili wameauawa katika ghasia hizo na wengine kiasi ya laki saba wameachwa bila makaazi tangu mwezi Desemba mwaka jana.Ban amesema zoezi la kupelekwa kwa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika taifa hilo iwapo kitaidhinishwa litachukua miezi kadhaa na raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hawana muda wa kusubiri.

Wanajeshi 12,000 wanahitajika CAR

Ban Ki-moon amependekeza vikosi vya kimataifa vya Umoja wa Afrika,Ufaransa na Umoja wa Ulaya viongezwe wanajeshi hadi kufika wanajeshi 12,000 na polisi katika wiki chache zijazo.

Wanajeshi wa Chad walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wanajeshi wa Chad walioko Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: MIGUEL MEDINA/AFP/Getty Images

Nyongeza hiyo ya wanajeshi itaziba pengo kwa hadi wiki sita hadi pale kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Mataifa kitakapoidhinishwa na baraza la usalama na kutumwa nchini humo.

Wanajeshi hao wa ziada wanapaswa kuangazia jinsi ya kukomesha ghasia, kuwalinda raia, kuzuia raia kuendelea kupoteza makaazi yao, kuhakikisha kuna mazingira salama ya kufikiswa kwa misaada ya dharura inakohitajika na kuweka msingi dhabiti wa kukabidhi madaraka kwa kikosi cha umoja wa Mataifa mapema iwezekanavyo.

Mkuu wa kushughulikia misaada ya kibinadamau wa umoja wa Mataifa Valerie Amos alisema hapo jana kwambaameshutushwa na alichokiona katika Jamhuri ya Afrika ya Kati alipokuwa katika ziara ya siku tatu nchini humo.Amos aliwaambia waandishi habari mjini Bangui baada ya kulizuru eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kuwa hakuna wanajeshi wa kutosha katika eneo hilo kudhibiti hali.

Wanajeshi walioko sasa wameshindwa kudhibiti hali

Wanajeshi wa Ufaransa na wa kikosi cha Umoja wa Afrika wamekuwa nchini humo kwa miezi kadhaa sasa lakini wameshindwa kudhibiti hali.Hata hivyo balozi wa Ufaransa katika umoja wa Mataifa Gerard Araud amesema vikosi hivyo viwili vimeanza kudhibiti hali.

Mkuu wa shughuli za kibinadaamu wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos
Mkuu wa shughuli za kibinadaamu wa Umoja wa Mataifa Valerie AmosPicha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Ulaya tayari umeanza kutuma wanajeshi wake 1,000 ili kujiunga na wanajeshi elfu sita wa umoja wa Afrika na 2,000 wa Ufaransa ambao wamekuwa wakijaribu kuzuia mzozo kati ya kundi la kiislamu na la kikiristo kuwa mbaya hata zaidi.

Ban ametaka usaidizi zaidi kutolewa kukipiga jeshi jeki kikosi cha umoja wa Afrika na pia kutolewa kwa dharura msaada wa kifedha kuisadia serikali kurejesha mifumo dhabiti ya asasi muhimu kama polisi,idara ya mahakama na magereza ili kujaribu kushughulikia masuala yanayoibuka kutokana na mzozo huo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman