1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ethiopia waonekana Somalia

Thelma Mwadzaya3 Februari 2009

Nchini Somalia vikosi vya jeshi la nchi jirani ya Ethiopia vinaripotiwa vimeonekana nchini humo ikiwa ni wiki moja tangu vikamilishe shughuli ya kuondoka rasmi.

https://p.dw.com/p/GmZQ
Rais mpya wa Somalia Sheikh Shariff Sheikh AhmedPicha: ap

Jeshi la Ethiopia lilishiriki katika operesheni ya pamoja ya kulinda amani nchini Somalia tangu mwaka 2006 kwa ushirikiano na jeshi la serikali ya muda ya Somalia.Kwa upande mwengine vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM vilivyoko mjini Mogadishu vinaripotiwa kuwapiga risasi raia 20 wa kawaida waliokuwa wakisafiri kwa mabasi.


Kwa mujibu wa wakazi wa eneo la mpaka wa Somalia na Ethiopia wanajeshi hao wa Ethiopia wameonekana kwenye upande wa Somalia wakiwa kwenye magari 17 ya kijeshi katika eneo la Kalabeyrka lililo kilomita chache kutoka upande wa Ethiopia wa mpaka.Ethiopia kwa upande wake imekanusha madai hayo kama anavyosisitiza Waziri wa Mawasiliano wa Ethiopia Bereket Simon.''Si kweli kwamba wanajeshi wa Ethiopia wamerejea nchini Somalia.Hakuna sababu ya msingi ya lawama hizo.Hatuna vikosi vyovyote nchini Somalia,shughuli ya wanajeshi hao kuondoka tayari imekamilika,wanajeshi wote wako katika ardhi ya Ethiopia.Kwa sasa hivi hatusimamii ujumbe wowote wa kijeshi nchini Somalia.''



Vikosi vya Ethiopia viliondoka rasmi nchini Somalia tarehe 25 mwezi uliyopita baada ya kukamilisha operesheni ya pamoja ya kulinda amani na vikosi vya serikali ya muda ya Somalia baada ya mahakama za kiislamu kuuteka mji wa Mogadishu kwa kipindi cha miezi 6 mwaka 2006.

Kwa upande mwengine naibu meya wa mji wa Mogadishu Abdifatah Shaweye ameunyoshea kidole ujumbe wa Umoja wa Afrika wa kulinda amani mjini humo AMISOM kwa kuwapiga risasi zaidi ya raia 20 wa kawaida waliokuwamo safarini kwenye mabasi.Tukio hilo lilitokea baada ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika kufyatua risasi pale waliposhambuliwa kwa bomu la kutegwa barabarani.Itakumbukwa kuwa ujumbe huo wa AMISOM unajumuisha vikosi vya Uganda na Burundi pekee.Kulingana na Waziri wa Ulinzi wa Uganda uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha tukio hilo na kuongeza kuwa huenda wapiganaji wa kundi la Al Shebab ndio waliohusika.

Kiongozi wa kundi la Al Shebab anaripotiwa kutoa wito kwa wapiganaji wake akiwataka kuongeza nguvu ya mashambulio yao dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AU.Sheikh Mukhtar Robow aliyasema hayo alipofanya mkutano na waandishi wa habari mjini Baidoa.

Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya rais mpya wa Somalia Sheikh Shariff Sheikh Ahmed kuapishwa rasmi baada ya uchaguzi uliofanyika kufuatia kujiuzulu kwa Abdullahi Yusuf Ahmed Disemba iliyopita.Rais Sheikh Shariff aliahidi kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na hasimu wake wa jadi Ethiopia.Ethiopia na Somalia zilipambana vitani katika miaka ya 1970.

Nchi ya Somalia imekuwa bila serikali thabiti tangu kungolewa madarakani kwa rais wa zamani Mohamed Siad Barre mwaka 1991.

Karibu watu milioni 3.25 nchini Somalia wanategemea msaada wa chakula kwasababu ya hali mbaya nchini humo.