1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Kenya wawaandama Al Shabab

Oumilkher Hamidou19 Oktoba 2011

Huku majeshi ya Kenya na somalia yakijitahidi kupambana na kundi la Al shabab katika ngome zao kusini mwa Somalia, Ufaransa imetangaza kifo cha raia wake aliyetekwa nyara na kundi hilo la wanamgambo.

https://p.dw.com/p/12vS8
Wanajeshi wa KenyaPicha: dapd

Marie Dadieu bibi wa miaka 66 mwenye asili ya kifaransa aliyetekwa nyara na al shabaab nchini kenya wiki chache zilizopita alifariki hii leo, akiwa mikononi mwa magaidi hao. Marie Dadieu alitekwa nyara kaskazini mwa Kenya karibu na mji wa Lamu.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Alain Juppe amesema bado hawajajua kiini kilichosababisha kifo chake lakini kutokana na hali yake ya kuugua saratani na ugonjwa wa moyo na kunyimwa dawa zake huenda ikawa ndio chanzo cha kifo chake.

Alain Juppe amelaani vikali tukio hili na kusema walifanya juhudi zote za kufikisha dawa za marehemu lakini kundi linaloshukiwa kumteka nyara la al shaabab wakakataa kupokea dawa hizo.

Frankreich Außenminister Alain Juppe
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Alain JuppéPicha: dapd

Kwengineko kulingana na msemaji wa jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir, majeshi yote ya Kenya na Somalia yamefanikiwa kuwauwa waasi 73 wa kundi la al shaabab katika mapigano hayo yalioingia siku yake ya nne hii leo.

Tayari majeshi hayo yamedhibiti miji mitatu. Kenya inasema vikosi vyake viko tayari kupambana na Al shaabab na kamwe haitasitisha mapigano haya mpaka wawakamate. Hata hivyo majeshi hayo yanakabiliwa na kibarua kigumu cha kusonga mbele katika miji inayoshikiliwa na al shaabab kutokana na mvua kali inayonyesha na kusababisha matope mazito.

Kwa upande wake kamanda mkuu nchini Somalia amesema lengo kuu ni kuingia katika bandari ya Kismayu ambayo ni kitovu cha Al shabaab. Generali Yusuf Hussein Dumaal ambaye ndio mkuu wa majeshi anayesimamia kusini mwa somalia,amesema wana nia ya kuwaangamiza al Shabab kuanzia bandari ya Kismayu hadi maeneo mengine ya Somalia.

Mji wa kismayu uko kilomita 120 kusini mashariki mwa mji wa Afmadow mahali yalipo majeshi kwa sasa.

Wakaazi mjini Afmadow wanasema, kwa sasa al shaabab wanawazuilia watu 22, wakiwemo wanawake 6 ambao wanashutumiwa na kundi hilo kwa kushirikiana na majeshi ya Kenya na Somalia. Ali Adow mkaazi wa eneo hilo amesema wana wasiwasi mkubwa wa hata kuwapigia simu jamaa zao kwa kuwa kundi la al shabaab linasikiliza kila simu kwa kushirikiana na wanaotoa huduma za simu mjini humo.

Sasa iwapo vikosi vya Kenya vitauteka mji wa Kismayu hii itakuwa pigo kubwa kwa Al Shabab, kwasababu mji huo ni kitovu cha oparesheni zao.

Karte Somalia Englisch
Ramani ya Kenya na Somalia

Kiongozi mkuu wa Al shabab Sheikh Hassan Dahir Aweys ameonya kuwa Kenya itajuta kwa kuingia Somalia. Amesema Kenya tayari imeingia katika orodha ya kushambuliwa na kuwa historia itajiandika pindi Al shabab watakapojibu mashambulizi.

Muandishi Amina Abubakar/RTRE

Mhariri Yusuf Saumu