1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa kulinda amani hatarini Cote d'Ivoire

1 Machi 2011

Umoja wa Mataifa wasema wanajeshi wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha kushambuliwa. Vikosi vya Gbagbo vyawashambulia wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa risasi

https://p.dw.com/p/10R1s
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa mjini AbidjanPicha: AP

Duru za Umoja wa Mataifa zimesema wataalamu hao na afisa mmoja wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, walikuwa wamekwenda katika uwanja wa ndege wa Yamoussoukro, kufuatia taarifa kwamba helikopta tatu za kivita zilikuwa zimetumwa kwa vikosi vya Gbagbo kutoka Belarus, kinyume na kikwazo cha silaha cha Umoja wa Mataifa kilichopitishwa mnamo mwaka 2004. Maafisa hao walilazimika kuondoka uwanjani hapo wakati walipofyatuliwa risasi. Hakuna majeraha yoyote yaliyoripotiwa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelitaka baraza la usalama la umoja huo likutane kwa dharura kujadili ukiukwaji wa kikwazo hicho cha silaha dhidi ya Cote d'Ivoire. Belarus imekanusha kuvunja sheria za Umoja wa Mataifa kuhusu vikwazo.

Kamati ya baraza la usalama inayoshughulikia vikwazo dhidi ya Cote d'Ivoire imekutana jana na kugundua kwamba madai dhidi ya Belarus hayajathibitishwa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa amedokeza kuwa madai hayo yalitolewa kwa misingi ya ripoti zilizopatikana na wataalamu wanaosimamia kikwazo hicho cha silaha. Msemaji wa ujumbe wa Ujerumani katika kamati hiyo amesema wameitaka tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire na jopo la watalaamu kuendelea kufuatilia hali nchini humo.

Mkutano wa Dakar

Wakati huo huo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire, Choi Young-Jin, amesema wanajeshi wa umoja huo wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha ukatili kutoka kwa vikosi vinavyomtii Laurent Gbagbo. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano na wajumbe wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika Magharibi mjini Dakar, Senegal, Choi Young-Jin amesema hali hii inazusha wasiwasi ikiwa Gbagbo amepoteza udhibiti wa vikosi vyake. Amesema kuna majaribio ya utekaji nyara na kuharibiwa kwa nyumba za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Elfenbeinküste Unruhen Dezember 2010
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Cote d'Ivoire Choi Young-jinPicha: AP

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo kumalizika, wajumbe wa Umoja wa Mataifa katika Afrika Magharibi wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya kuzorota kwa hali nchini Cote d'Ivoire na athari zinazoweza kutokea. Wamezungumzia hususan idadi kubwa ya wakimbizi inayozidi kuongezeka, huku Umoja wa Mataifa ukikadiria wakimbizi takriban 70,000 wamekimbilia nchi jirani ya Liberia. Watu wapatao 1,800 waliokimbia mapigano mwishoni mwa juma lililopita wamepata hifadhi katika kanisa moja la Katoliki katika kitongoji cha Abobo kaskazini mwa nchi. Wengine takriban 1,000 wanaishi katika kanisa la Anyama katika eneo la kaskazini.

Utekaji nyara

Hapo jana vijana watiifu kwa rais Gbagbo waliwateka nyara wafanyakazi wawili wa tume ya Umoja wa Mataifa lakini baadaye wakawaachia. Msemaji wa tume hiyo, Hamadoun Toure amesema wawili hao walitekwa karibu na kitongoji cha Port Bout na baadaye kukabidhiwa kwa kikosi cha Gbagbo cha FDS. Waliachiwa wakati tume ya Umoja wa Mataifa ilipozungumza na kikosi hicho.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Aboubakar Liongo