1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroJordan

Jordan: Wanajeshi watatu wa Marekani wauawa katika shambulio

29 Januari 2024

Wanajeshi watatu wa Marekani wameuawa na wengine karibu 34 wamejeruhiwa katika shambulio la droni kaskazini-mashariki mwa Jordan karibu na mpaka wa Syria.

https://p.dw.com/p/4bmng
Picha ya satelaiti- Kambi ya Jeshi la Marekani kaskazini mwa Jordan
Kambi ya Jeshi la Marekani inayofahamika kama "Tower 22" iliyoshambuliwa kaskazini mwa JordanPicha: Planet Labs PBC/picture alliance

Tukio hilo linadaiwa kuendeshwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran. Taarifa hiyo imetolewa jana na maafisa wa Marekani na kuthibitishwa na Rais Joe Biden ambaye ameapa kujibu shambulio hilo.

Biden amelaani vitendo vya wanamgambo hao wanaoungwa mkono na Iran kwa kuhusika na tukio la kwanza lililosababisha vifo vya askari wa Marekani baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya makundi kama hayo huko Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa mzozo wa Israel na kundi la Hamas.

Soma piaIran yalaaniwa vikali katika kura ya Baraza la Usalama

Biden amesema katika taarifa yake kwamba Marekani itawawajibisha kwa wakati na kwa namna watakaoamua wao wale wote waliohusika na shambulio hilo huku Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin akisisitiza kuwa watachukua hatua zote zinazohitajika ili kutetea maslahi ya Marekani na kuwalinda wanajeshi wao.

Waziri wa Ulinzi Wa Marekani Lloyd Austin
Waziri wa Ulinzi Wa Marekani Lloyd Austin ameapa kuwa nchi yake itafanya kila waliwezalo kulinda maslahi yao.Picha: Violeta Santos Moura/REUTERS

Huku kukiwa na hatari inayoongezeka ya kutanuka kwa mzozo wa kijeshi katika eneo hilo, maafisa wa Marekani wanashughulika kubaini hasa kundi lililohusika na shambulio hilo, lakini wametathmini kwamba moja ya makundi kadhaa yanayoungwa mkono na Iran ndilo lililoendesha tukio hilo.

Iran yakanusha kuhusika na shambulio hilo

Iran imetupilia mbali kuhusika kwa namna yeyote na shambulio hilo. Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje Nasser Kanaani amesema leo hii kuwa madai kama hayo "hayana msingi wowote," na kwamba  "vikundi vya ukombozi" havipewi maagizo kutoka kwa Jamhuri ya Kiislam ya Iran. Kanaani ameongeza pia kuwa kuendelea kwa mashambulizi ya Marekani nchini Syria na Iraq pamoja na vita vya Gaza vitazidisha hali ya ukosefu wa utulivu katika ukanda huo.

Khaled Al Qudah ni raia wa Jordan na ametoa mtazamo wake kuhusu shambulio hilo:

" Jordan ilifahamu kabisa kwamba kadri Marekani itakavyoendelea kuiunga mkono Israel kwenye vita vyake katika ukanda wa Gaza, hii itasababisha mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya Marekani katika eneo hili, na kutakuwa na hisia za kuunga mkono vikundi vya ukombozi. Kujihusisha kwa Jordan katika mzozo huo hakuwezi kuiepusha na athari kama hizi za mashambulizi ya droni au majibu yoyote ya kijeshi sehemu mbalimbali."

 Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Iran- Nasser Kanaani
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Iran Nasser Kanaani amekanusha kuhusika kwa nchi yake katika shambulio hilo.Picha: Iranian Foreign Ministry/Zuma/picture alliance

Wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran mashariki mwa Syria wameanza kuondoka wakihofia mashambulizi ya anga ya Marekani.  Hayo ni kwa mujibu wa mwanaharakati mwenye makazi yake Ulaya ambaye anaongoza chombo cha habari cha Deir Ezzor 24 Omar Abu Layla ambaye ameliambia shirika la habari la AP kwamba makundi hayo yameondoka katika ngome zao huko Mayadeen na Boukamal.

Soma pia: Iraq yalaani mashambulizi ya Marekani

Kamandi kuu ya jeshi la Marekani imesema takriban wanajeshi 350 walipelekwa eneo hilo lililopo kwenye mpaka wa Syria na kwa kiasi kikubwa, hushiriki katika misheni ya ushauri na usaidizi kwa vikosi vya Jordan. Kambi ya jeshi la Marekani ya al-Tanf nchini Syria inapatikana takriban kilomita 20.

Kituo kilichoshambuliwa cha Jordan ni sehemu muhimu ya usambazaji wa vifaa kwa vikosi vingine vya Makrekani vilivyopo nchini Syria, ikiwemo kambi ya al-Tanf, ambayo iko karibu na mpaka wa Iraq, Syria na Jordan.

(rtre,ape)